WAKAZI wa kijiji cha Makatani kata ya Kagugu Halmashauri ya Mji Mbinga mkoani Ruvuma,wanatarajia kuondokana na adha ya kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 25 kila siku kwenda kata jirani ya Tingi kufuata huduma za afya.
Wakazi hao wamepata matumani mapya baada ofisi ya Mkurugenzi wa mji Mbinga kuingilia kati na kuanza kukamilisha ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho iliyoanza kujengwa zaidi ya miaka 17 bila kukamilika.
Diwani wa kata ya Kagugu Batson Mpogolo amesema, zahanati hiyo ilianza kujengwa mwaka 2006 kwa nguvu za wananchi lakini ujenzi wake ulisimama kutokana na kukosa fedha za kukamilisha ili huduma ziweze kutolewa.
Mpogolo ameishukuru Halmashauri ya Mji Mbinga kutoa fedha kwa ajili ya kukamilisha kazi ya ujenzi wa zahanati hiyo ambayo imekamilika kwa asilimia 95.
Kwa mujibu wa Mpogolo, kazi zilizobaki katika ujenzi huo ni kuchimba matundo ya vyoo na kujenga kichomea taka na kuwaomba wananchi wa kata hiyo kuendelea kuvuta subira wakati huu ambao serikali iko hatua za mwisho kukamilisha ujenzi wa zahanati hiyo.
Hata hivyo,ameiomba serikali kuharakisha kwa kuleta vifaa tiba na wahudumu ili zahanati iweze kuhudumia wananchi ambao bado wanaendelea kuteseka kwa kwenda maeneo mengine kufuata huduma za afya.
Mtendaji kata wa Kagugu John Makoyole amesema,kata ya Kagugu yenye zaidi ya wakazi 1,820 kuna zahanati moja tu ya Makatani ambayo bado haijaanza kufanya kazi,hivyo wananchi wanalazimika kwenda kata nyingine kufuata huduma.
Amesema,hali hiyo imesababisha wananchi wengi kuwa maskini kwa kuwa wanakosa muda wa kufanya kazi za maendeleo,badala yake wanatumia muda mwingi kwenda maeneo mengine kufuata huduma za afya.Ameishuru serikali kwa uamuzi wake wa kumalizia kazi ya ujenzi wa zahanati hiyo ili wananchi wapate huduma za afya karibu na maeneo.
Aidha,ameipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kuboresha baadhi ya huduma za kijamii ikiwamo maji,barabara na nishati ya umeme ambapo kati ya vijiji vitano vya kata hiyo,vitatu vimefikiwa na umeme.
Eliza Mapunda mkazi wa kijiji hicho amesema,kukamilika kwa zahanati kutawezesha kuanza kutumika na kupunguza gharama walizokuwa wakitumia kusafiri kwenda mbali kufuata huduma za afya zinazopatikana kata za jirani na Hospitali ya wilaya Mbinga mjini.
Amesema,kwa sasa wanalazimika kutumia gharama kubwa kati ya shilingi 10,000 hadi 15,000 kwa usafiri wa boda boda kwenda kata ya Tingi kupata matibabu jambo lililowatesa kwa muda mrefu.
Mkazi mwingine Mathias Sangana amesema, kukamilika kwa zahanati hiyo italeta hamasa kubwa kwa akina mama wajawazito kuanza kliniki mapema na kujifungulia Hospitali kuliko sasa ambapo wajawazito wengi wanachelewa kuhudhuria kliniki mapema kutokana na gharama kubwa ya usafiri.
Kwa upande wake mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Mbinga Dkt Maximo Magehema amesema,serikali kupitia Halmashauri yam ji Mbinga iko hatua ya mwisho kukamilisha ujenzi wake.
Amesema,mara baada ya kazi za ujenzi zitakapokamilika itapeleka vifaa tib ana watumishi ili iweze kuanza kutoa huduma kwa wananchi wa kijiji cha Makatani na kata nzima ya Kagugu.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.