BAADHI ya Wananchi wa mtaa wa Kipika kata ya Matarawe Halmashauri ya mji Mbinga mkoani Ruvuma,wameiomba serikali kukamilisha haraka ujenzi wa zahanati yao ili waweze kuondokana na adha wanayoipata ya kufuata matibabu mbali na makazi yao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wamesema, kwa sasa ujenzi wa zahanati hiyo umesimama kutokana na kukosekana kwa fedha, hivyo wameiomba serikali kutafuta mbinu mbadala ambazo zitawezesha kukamilika kwa ujenzi huo.
Amina Pili amesema,kwa muda muda mrefu wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma za afya na wakati mwingine akina mama wajawazito wanajifungulia njiani wakati wakifuata huduma na kuingia gharama kubwa ya usafiri hasa nyakati za usiku.
Amesema,wananchi wa mtaa huo kwa kiasi kikubwa wanategemea kupata huduma katika Hospitali ya wilaya Mbuyula pekee iliyopo umbali wa km 5 na hakuna njia mbadala,jambo linalo sababisha baadhi yao kushindwa kuwahi katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa wakati na hivyo kupoteza maisha yao.
Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa KipikaThomas Mahundi,ameipongeza Halmashauri ya mji Mbinga kuona umuhimu wa kupeleka ujenzi wa zahanati hiyo ambayo itamaliza kero na usumbufu kwa wananchi wa mtaa wa Kipika na kata ya Matarawe kwenda maeneo mengine kufuata huduma za afya.
Amesema,zahanati hiyo itakapokamilika itawezesha na kusaidia kupunguza foleni ya wagonjwa katika Hospitali ya wilaya Mbinga,na kuiomba serikali kufanya haraka kukamilisha zahanati hiyo ambayo itakuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi.
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya mji Mbinga Dkt Maximo Magehema amesema, ujenzi wa zahanati hiyo umefikia asilimia 98 na gharama za ujenzi wake ni Sh.milioni 93 kati ya hizo shilingi milioni 62 zimeshatumika.
Dkt Magehema amesema,zahanati hiyo itakapokamilika itasaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa katika Hospitali ya mji Mbinga na kusaidia kusogeza huduma za afya kwa wananchi wa kata ya Matarawe.
Ameeleza kuwa,zahanati hiyo itawezesha wananchi kupata huduma karibu na makazi yao na watoto wadogo kupata huduma muhimu za chanjo,badala ya wazazi wao kulazimika kwenda mbali kwa ajili ya huduma hizo.
Aidha,amewataka wananchi wa kata hiyo kupenda kushiriki na kuchangia nguvu zao katika shughuli mbalimbali za maendeleo,badala ya kuichia serikali peke yake kwani kufanya hivyo itasaidia miradi inayoibuliwa na kutekelezwa kukamilika kwa wakati.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Mbinga Grace Quintine amesema,kwa mwaka wa fedha 2022/2023 wamepokea kiasi cha shilingi milioni 150 kutoka serikali kuu zilizotumika kujenga zahanati tatu ikiwamo ya kata ya Matarawe ambayo ujenzi wako uko hatua ya mwisho kukamilika.
Quintine amesema,zahanati hiyo na nyingine zitakapomilika zitasaidia kutatua changamoto ya wananchi wa maeneo husika kutembea umbali mrefu na kutumia muda mwingi kwenda maeneo mengine kufuata huduma za afya.
Aidha amesema, Halmashauri ya Mji Mbinga kutoka mapato ya ndani imetenga na kutumia shilingi milioni 89 zilizofanikisha kujenga zahanati mbili ambazo zimekamilika na kuanza kutoa huduma za afya kwa wananchi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.