BAADHI ya wananchi wa kata ya Luwaita Halmashauri ya mji Mbinga wilayani Mbinga,wameiomba serikali kupitia Halmashauri ya Mji Mbinga,kukamilisha ujenzi wa zahanati ya Luwaita kutokana na ujenzi wake kuchukua zaidi ya miaka 5 bila kukamilika.
Wamesema kukosekana kwa huduma za afya katika kata hiyo,kumesababisha akina mama wajawazito kulazimika kujifungulia njiani kutokana na vituo vya afya vilivyopo kuwa umbali wa zaidi ya kilomita 7 kutoka katika maeneo wanayoishi.
Wameiomba Halmashauri ya mji Mbinga ,kuwahurumia kutokana na mateso wanayopata kutumia muda mwingi kwenda kupata huduma maeneo mengine kwa kuanza mchakato wa kufungua na kutoa baadhi ya huduma katika zahanati hiyo ambayo sehemu kubwa ujenzi wake umekamilika.
Bosco Komba amesema, zahanati hiyo ilianza kujengwa kwa muda mrefu kwa wananchi kuchangia nguvu zao ili waweze kupata huduma za matibabu karibu,hata hivyo wanashangazwa na ukimya wa serikali kushindwa kufungua na kutoa huduma kwa wananchi.
Maria Nchimbi amesema,wananchi wa kata ya Luwaita wanatamani kuona zahanati hiyo ikianza kutoa huduma kwani wamechoka kuvumilia kutembea umbali mrefu kila wanapohitji kupata huduma za matibabu ambazo zinapatikana kwenye vituo vilivyopo mbali na makazi yao.
Mtendaji wa kijiji cha Luwaita Rehema Ameir ameeleza kuwa,awali mpango wa serikali ulikuwa kituo cha afya,lakini kukosekana kwa nguvu kazi za wananchi ikaamua iwe zahanati kwa kuwa zilihitajika nguvu za pamoja kati ya serikali na wananchi wa eneo husika.
Hata hivyo amesema,ujenzi wa zahanati ya Luwaita umekamilika kwa asilimia 99 na wakazi zaidi ya 4,000 wanatarajia kupata huduma mara itakapoanza kutoa huduma,lakini kuchelewa kufunguliwa kunatokana na kukosekana kwa vyoo na kichomea taka.
Amesema,zahanati hiyo itarahisisha upatikanaji wa huduma na kuwaondolea wananchi adha ya kusafiri umbali mrefu kwenda kutafuta huduma kwenye vituo vingine vya afya na kupunguza muda mwingi wanaopaswa kujikita katika shughuli za maendeleo.
Kwa upande wake kaimu mganga mkuu wa Halmashauri ya mji Mbinga Dkt Maximo Magehema amesema,kimsingi zahanati hiyo imekamilika na serikali ipo katika hatua ya mwisho kuanza kutoa huduma na kuwaomba wananchi kuwa wavumilivu wakati serikali ikikamilisha mambo muhimu ya kiutendaji ikiwamo vifaa na watumishi.
Amesema,serikali ya awamu ya sita kupitia Halmashauri ya mji Mbinga imejipanga kuhakikisha kila kijiji kina zahanati na kata kituo cha afya ili kusogeza na kuboresha huduma za afya kwa wananchi wake.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.