Maafisa Ardhi wa Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma wamewataka wananchi kuchangamkia fursa ya punguzo la asilimia 42.9 ya bei ya umilikishwaji wa ardhi baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoa ofa hiyo.
Afisa Ardhi Mteule wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga France Kaganda, alieleza kuwa kuanzia Julai Mosi, 2023, gharama zimepungua kutoka Shilingi 163,000 hadi Shilingi 93,000 kwa kiwanja chenye mita za mraba 600.
Bw. Kaganda alikuwa anazungumza wakati kwenye kilele cha kampeni maalum ya siku nne ya kutoa elimu ya masuala yahusuyo usimamizi wa sheria, kanuni na taratibu za uendelezaji wa ardhi, kusikiliza na kutatua migogoro ya ardhi katika Wilaya ya Mbinga.
"Tunawataka wananchi wote wenye viwanja ambavyo vimepimwa na vina sifa ya kuandaliwa hati kujitokeza ili kupata nyaraka za hati miliki," alisema Bw. Kaganda.
Aliongeza kuwa mwananchi akilipa kodi ya ardhi na kupeleka vithibitisho vyote katika idara ya Ardhi, ataandaliwa na kupatiwa hati yake ndani ya siku 14.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mhe. Aziza Mangosongo aliwataka maafisa Ardhi kutoa hati miliki kwa wakati ili watu waanze shughuli za ujenzi kwa wale wanaohitaji kujenga.
Aliwaasa wananchi kufuata ushauri wa wataalamu wa ardhi ili kuepuka athari mbalimbali zinazoweza kujitokeza baadae ikiwa ni pamoja na kubomolewa nyumba au kupitiwa na mafuriko.
"Watu wengi wamekuwa wakipigana na kuumizana kutokana na migogoro ya ardhi, ninakiagiza kitengo cha Ardhi kuwa wasuluhishi zaidi kuliko kuwa chanzo cha migogoro," aliagiza Mhe. Aziza
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga Bi. Amina Seif alisema kuwaona wataalamu wa ardhi na kupata hati miliki pamoja na ushauri itasaidia kupunguza au kuondoa migogoro ya ardhi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.