WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS),umewataka wananchi hususani wanaojishughulisha na kilimo kuacha kutumia moto kama njia ya kusafisha mashamba yao.
Badala yake wameshauriwa kutumia mbinu mbadala ikiwemo majembe na zana nyingine ili kuepusha uharibifu wa mazingira unaoweza kusababisha majanga ya moto katika misitu na uoto wa asili.
Wito huo umetolewa na Mhifadhi Misitu Mwandamizi wa TFS John Kimolo, wakati akizungumza na Waandishi wa Habari waliotembelea shamba la miti Mpepo kata ya Mpepo wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma.
Amesema,wakulima wanapotaka kuandaa na kusafisha mashamba yao wanapaswa kuchukua tahadhari na kupata ushauri wa kitaalamu ili kuepuka kutokea kwa majanga ya moto katika misitu ya asili na miti ya kupandwa na maeneo ya uoto wa asili.
“wananchi wanapoandaa mashamba yao wanatakiwa kufyeka nyasi na miti na kukusanya mabiwi na wachome kwa kuzingatia mwelekeo wa upepo,sisi kama shamba la miti Mpepo tutaendelea kutoa elimu juu ya kuzingatia utumiaji sahihi wa moto kwenye mashamba”alisema Kimolo.
Amesema,Shamba la miti Mpepo limeanzisha bustani ya miti ambayo inapandwa kwenye mashamba ya Serikali,taasisi za Serikali na kugawa miche ya miti kwa watu binafsi ili waweze kupande katika maeneo yao kwa ajili ya kujiongezea kipato.
Kwa mujibu wa Kimolo,katika bustani hiyo miche ya miti inayooteshwa ni jamii ya misindano inayopandwa mahususi kwenye mashamba yaliyopo safu za Mpepo,Kivulungwa na Lusewa ambazo zinastawi vizuri miti.
Amesema,safu na Liuli zilizopo pembezoni mwa ziwa Nyasa imepandwa miti ya aina ya misaji(tiki)inayostawi vizuri kwenye ukanda wa chini.
Diwani wa Kata ya Mpepo Mheshimiwa Anderson Haule amesema,tangu Serikali kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ilipoanzisha mradi wa upandaji miti umesaidia wananchi wa kata hiyo kupata ajira za muda na wengine ajira za kudumu na hivyo kupunguza tatizo la ajira hasa kwa vijana na wanawake.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.