Wananchi wa mitaa ya Namakinga na Dodoma, katika Kata ya Maposeni na Peramiho, mkoani Ruvuma, wamepokea kwa shukrani mradi wa ujazilizi wa umeme kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA). Wakazi wa maeneo hayo wamesema mradi huu utaboresha maisha yao kwa kuwawezesha kupata huduma za kijamii na fursa za kiuchumi.
Afisa Habari na Uhusiano wa TANESCO mkoani Ruvuma, Allan Njiro, amewatembelea wananchi hao na kuwapa elimu kuhusu taratibu za kupata huduma ya umeme. Ameeleza kuwa wananchi wanaounganishiwa umeme kwa matumizi ya nyumbani wanapaswa kulipa shilingi 27,000, huku wale wa matumizi ya viwanda wakilipa shilingi 139,000.
Aidha, Njiro amefafanua kuwa ili kuunganishiwa umeme, wananchi wanapaswa kufanya maombi kwa njia ya simu, kuwa na kitambulisho cha NIDA, kuhakikisha nyumba zao zimefanyiwa wiring na mkandarasi, na kuhakiki uwepo wa nguzo za umeme. Amesisitiza kuwa ada ya kuunganishiwa umeme inabaki kuwa bure, huku gharama za vifaa vya ndani zikibebwa na wananchi wenyewe.
Kwa upande wake, Kaimu Afisa Habari wa Huduma kwa Wateja, Emma Ulendo, amewahimiza wananchi kutumia fursa hii kwa manufaa ya jamii. Amesema kuwa gharama za kuunganishiwa umeme kwa wananchi wa Songea Vijijini ni shilingi 27,000, huku wale wa mijini wakitakiwa kulipa shilingi 321,000. Amehimiza wakazi kuhakikisha nyumba zao zinafanyiwa wiring kwa viwango sahihi ili kuepuka hatari za umeme.
Diwani wa Kata ya Maposeni, Monica Tambara, ameipongeza TANESCO kwa kutoa elimu kuhusu utunzaji wa miundombinu ya umeme. Pia, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuhakikisha wananchi wanapata umeme kwa gharama nafuu na kumpongeza Mbunge wa Songea Vijijini, Jenista Mhagama, kwa kuendeleza maendeleo ya eneo hilo.
Serikali imeendelea kusisitiza ushirikiano wa wananchi katika kuutunza mradi huu wa REA ili kuhakikisha unawanufaisha kwa muda mrefu. Mradi huu unatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika sekta za biashara, elimu na afya, hivyo kuchochea maendeleo kwa wananchi wa Namakinga na Dodoma.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.