IDADI ya watu katika mkoa wa Ruvuma imeongezeka kutoka watu milioni 1,376,891 mwaka 2012,hadi kufikia 1,848,794 sawa na ongezeko la watu 471,903 katika kipindi cha miaka kumi.
Idadi hiyo inaonyesha kiwango cha ukuaji wa watu katika mkoa huo kimeongezeka kutoka asilimia 2.1 hadi asilimia 2.9 ikiwa ni chini ya kiwango cha kasi ya ongezeko la idadi ya watu kitaifa ambayo ni asilimia 3.2 kwa mwaka 2022.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa mkoa hu Kanal Laban Thomas,wakati akifungua semina ya uwasilishaji,usambazaji na uhamasishaji matumizi ya matokeo ya Sensa kwa viongozi na watendaji wa mkoa wa Ruvuma iliyofanyika katika ukumbi wa Parokia ya Bombambili mjini Songea.
Alisema kutokana na kasi kubwa ya ongezeko la watu,viongozi wa mkoa huo wanapaswa kujipanga vyema na kuweka mikakati madhubuti na endelevu kwa kutoa huduma bora za kijamii na za kiuchumi kwa wananchi ili kuimarisha ustawi wao na maendeleo ya mkoa huo.
Kanal Laban,amewataka viongozi na watendaji kuhakikisha kuwa mipango yao ya maendeleo ya muda mfupi,muda wa kati na muda mrefu yanazingatia idadi ya watu,mahitaji yao na mazingira wanayoishi inazingatia matokeo ya Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.
Ametaka mipango hiyo izingatie mwenendo wa ongezeko la kasi ya ukuaji wa idadi ya watu ili mkoa huo unakuwa miongoni mwa mikoa ya mfano katika matumizi ya takwimu zilizotolewa na Ofisi ya taifa ya Takwimu nchini.
Aidha amewaasa viongozi na watendaji katika ngazi zote za kiutawala katika mkoa huo,kuhakikisha wanasimamia vyema maendeleo na kugawa rasilimali za taifa kwa kufuata vigezo vya kitakwimu,badala ya kugawa kwa upendeleo.
Ametaka,matumizi mazuri ya matokeo ya sensa katika kufanya maamuzi yenye kufuata vigezo vya kitakwimu na kuepuka kufuata au kutekeleza matakwa binafsi au maagizo ya baadhi ya watu binfasi.
Kanal Laban,amewapongeza na kuwashukuru viongozi na watendaji kuanzia ngazi ya mkoa,mitaa,vitongoji na wananchi wa mkoa huo kwa ushirikiano na mshikamano walionesha wakati wa mchakato mzima wa maandalizi ya sensa hadi kukamilika tarehe 5 Septemba 2022.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania Dkt Albina Chuwa, Mratibu wa Sensa ya watu na makazi mkoa wa Ruvuma Mwamtumu Athuman alisema,semina hiyo inalenga kuongeza uwezo wa kuwafahamisha na kuwaelimisha wananchi namna ya kupata matokeo ya sensa na kuyatumia katika shughuli zao binafsi za kuinua hali zao za maisha
Alisema,uelewa mzuri wa wananchi wa matumizi ya matokeo ya sensa utasaidia sana kutoa mchango wao katika maendeleo ya Taifa kwa kushiriki vyema,kufanya maamuzi na kufuatilia utekelezaji wa shughuli za maendeleo zinazofanywa na Serikali na wadau wengine wa maendeleo.
Pia alisema,hatua hiyo itasaidia kuongeza uwajibikaji kwa watendaji na viongozi wa kuchaguliwa wakiwemo Wabunge na madiwani ambao wanapaswa kuyaelewa na kuyatumia matokeo ya sensa ya mwaka 2022 kama dira katika kufanya maamuzi yanayohusu maendeleo ya wananchi.
Athuman,ameipongeza wilaya ya Tunduru kwa kufanya vizuri katika sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 na kuwaomba wadau wote kupeleka maombi au maoni ofisi ya Taifa ya Takwimu kuhusiana na matokeo ya zoezi la sensa ya watu na makazi ili yaweze kufanyiwa kazi.
Naye Mratibu wa Sensa Taifa Seif Kuchengo alisema,katika mkoa wa Ruvuma wilaya inayoongoza kuwa na idadi kubwa ya watu ni Tunduru yenye jumla ya watu laki 4.12 ikifuatiwa na Manispaa ya Songea yenye watu laki 2.86 na Halmashauri ya mwisho Madaba yenye wakazi elfu 65,215.
Aliongeza kuwa,idadi hiyo inaifanya Halmashauri ya wilaya Tunduru kuwa na zaidi ya asilimia 23.6 ya watu wote wa mkoa wa Ruvuma na Halmashauri ya Madaba kuwa na asilimia 3 tu ya wakazi wote wa mkoa wa Ruvuma.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.