Na Albano Midelo,Songea
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas ametoa rai kwa wananchi kushiriki kikamilifu kutoa maoni katika maandalizi ya Dira mpya ya maendeleo ya 2050.
Kanali Thomas ametoa rai hiyo wakati anafungua mafunzo ya matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kwa viongozi na watendaji wa Mkoa,Kamati ya Sensa ya Mkoa,wadau na makundi maalum katika jamii yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Parokia ya Bombambili mjini Songea.
Amesema Dira ya maendeleo ya 2025 inaelekea ukingoni ambapo serikali inaandaa Dira mpya ya 2050 ambapo ameshauri kutumia matokeo ya Sensa ya 2022 na t takwimu nyingine katika kutoa maoni na mapendekezo.
“Hatuna budi kutoa maoni yetu kwa Tanzania tunayoitarajia ifikapo mwaka 2050,tuna bahati serikali yetu imetuwekea njia mbalimbali za kutuwezesha kutoa maoni na mapendekezo yetu’’,alisisitiza RC Thomas.
Akizungumzia mafunzo hayo,Mkuu wa Mkoa amesema semina hiyo ni mfululizo wa mafunzo ya usambazaji na uhamasishaji wa matumizi ya matokeo ya sensa ya mwaka 2022 kama ilivyoelekezwa kwenye Mwongozo wa kitaifa wa matumizi ya matokeo ya sensa uliozinduliwa Oktoba 2022 na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan wakati anazindua matokeo ya mwanzo ya sensa.
Mkuu wa Mkoa ameipongeza serikali ya Awamu ya Sita kwa kuandaa Mwongozo huo ambao unaimarisha uwezo wa viongozi na wananchi katika kupanga,kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa mipango na program za maendeleo.
Ameyataja mafunzo hayo kuwa yana umuhimu wa kipekee kwa washiriki kwa sababu yatawawezesha kutekeleza majukumu ya uongozi na utendaji kwa umakini,weledi,na usahihi zaidi hivyo kuharakisha maendeleo ya Mkoa.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mtakwimu Mkuu wa Serikali Mwantumu Athuman ameyataja malengo ya mafunzo hayo kuwa ni kuwajengea wadau uwezo wa kutafsiri,kuchambua na kuyatumia matokeo ya Sensa katika kupanga,kutekeleza,kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa sera,mipango na program mbalimbali za maendeleo.
Amesisitiza kuwa utekelezaji wa Sensa ya watu na makazi ni uwekezaji mkubwa unaofanywa na serikali ili kupata taarifa muhimu na za msingi kuhusu watu wake, kidemografia ,kiuchumi na kimazingira.
Hata hivyo ameyataja madhumuni ya kupata taarifa hizo ni kuzitumia kwa kuhuisha sera,kupanga mipango na program za maendeleo na kufuatilia utekelezaji wake.
Ameitaja moja ya faida kubwa ya matumizi sahihi ya matokeo ya Sensa ni kuongeza ufanisi katika matumizi ya rasilimali za nchi kwa kufanya maamuzi yanayohusu maendeleo ya nchi kwa kuzingatia idadi ya watu,mahitaji yao na mazingira wanamoishi.
Kaulimbiu ya awamu ya tatu ya utekelezaji wa sensa ni Matokeo ya Sensa ya Sita,Mipango Jumuishi kwa Maendeleo Endelevu.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.