Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed amewaasa wadau na wananchi kujitokeza kwenye zoezi la uandikishaji wapiga kura ambalo linafanyika kwa siku kumi kuanza Oktoba 11 hadi 20 mwaka huu.
Kanali Abbas Ametoa rai hiyo wakati anafungua kikao cha wadau wa uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2024 kilichofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea .
“Sina shaka kila mmoja wetu anajua kuwa mafanikio ya uchaguzi huu yanategemea sana ni kwa kiwango gani wananchi wetu watakuwa wamejiandikisha,matarajio yangu ni kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Songea mtahamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha ili wananchi wote wajiandikishe’’,alisisitiza.
Amewaasa wadau wa uchaguzi kuhakikisha eneo hilo linafanikiwa hali ambayo itawezesha maeneo mengine ya kampeni na siku ya kupiga kura kupata mafanikio mazuri.
Katika kikao hicho wadau muhimu wakiwemo maafisa watendaji wa mitaa na kata kutoka Manispaa ya Songea wameshiriki,ambapo Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma amewaasa watendaji hao kuhakikisha wanakuwa waadilifu katika kazi hiyo na kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni na miongozo ya uchaguzi.
Kanali Abbas amewatahadharisha watendaji hao kujiepusha na tabia zinazoweza kusababisha kuwa wazembe ili kazi hiyo iweze kufanyika kikamilifu kama ilivyotarajiwa.
Awali akizungumza kwenye kikao hicho,Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Furaha Mwangakala amesema katika Halmashauri hiyo mitaa 123 itashiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa ili kuwapata viongozi katika ngazi hiyo.
Amesema Halmashauri inaendelea na maandalizi kabla ya uchaguzi ambapo hadi sasa elimu na uhamasishaji unaendelea kufanyika kupitia vyombo vya Habari,mabango,matangazo barabarani (PA) na mikutano ya hadhara.
Kaulimbiu ya uchaguzi wa serikali za mitaa kwa mwaka huu inasema serikali za mitaa sauti ya wananchi jitokeze kushiriki uchaguzi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.