WANANCHI wa vijiji vinavyopitiwa na Barabara ya Likuyufusi –Mkenda na nchi jirani ya Msumbuji kwa upande wa mkoa wa Ruvuma,wameiomba Serikali kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami ili kutatua changamoto za usafiri wa abiria na mizigo hususani katika kipindi cha masika.
Wametoa ombi hilo kwa nyakati tofauti mbele ya waandishi wa Habari wa mkoa wa Ruvuma walioko kwenye ziara ya kutembelea miradi ya barabara inayotarajia kutekelezwa na inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita kupitia wakala wa barabara Tanzania(TANROADS) katika mkoa wa Ruvuma.
Shaban Kilomoni mkazi wa kijiji cha Nakawale wilayani Songea alisema,katika wilaya hiyo kuna fursa nyingi ikiwamo makaa ya mawe,hata hivyo bado hayajaanza kuchimbwa wala kunufaisha serikali kutokana na tatizo kubwa la miundombinu ya barabara.
Alisema licha ya rasilimali nyingi zinazopatikana wilayani humo,wawekezaji na wafanyabiashara wameshindwa kufika kutokana na ubovu wa barabara hiyo,jambo linalochelewa sana maendeleo yao.
“kukosekana kwa barabara ya lami ni chanzo cha kusua sua kwa maendeleo kwenye maeneo yetu,hali hii imechangia sana hata usafiri kwenda Songea mjini huwa ngumu siyo wakati wa masika tu bali hata muda wa kiangazi, na madereva wanatumia nafasi hiyo kupandisha nauli kutoka Sh.3000 hadi 7000”alisema.
Kandedus Mbawala dereva wa basi linalofanya safari zake kati ya Songea mjini na Mkenda darajani alieleza kuwa,wakati wa masika wanalazimika kutumia kati ya masaa 3 hadi 4 kufika Songea mjini na kama ingejengwa kwa lami muda huo ungepungua hadi saa 1.
Alisema kuwa,iwapo Serikali itajenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami basi itaharakisha kukua kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja,wilaya,mkoa na nchi kwa ujumla.
Hata hivyo, ameipongeza TANROADS kujenga barabara hiyo kwa changarawe,hali iliyo rahisisha huduma ya usafiri na usafirishaji kuendelea japo kwa shida wakati huu ambao serikali iko kwenye maandalizi ya kujenga kwa kiwango cha lami.
Mrakibu wa Uhamiaji wa kituo cha Mkenda Upendo Kikudo,alisema, watumishi wa serikali ni sehemu ya waathirika wakubwa wa ubovu wa barabara hiyo kwani wanapohitaji kwenda makao makuu ya wilaya na mkoa kikazi, wanalazimika kutumia muda mrefu na hivyo kuathiri shughuli za kuwahudumia wananchi.
Aidha,ameishukuru Serikali kwa kuonyesha nia ya kutaka kujenga barabara hiyo ambayo ni muhimu kwa uchumi wa nchi yetu na nchi jirani ya Msumbiji.
Kwa mujibu wa Kikudo,barabara hiyo ni muhimu na kama itajengwa kwa lami itatumika kikamilifu kusafirisha bidhaa kutoka Bandari ya Mtwara kwenda nchi jirani ya Msumbuji kwa kutumia kituo cha forodha cha Mkenda.
Alisema, kwa sasa wafanyabiashara wengi wa Msumbiji wanalazimika kutumia bandari ya Dar es slaam na hatimaye kupita mpaka wa Tunduma mkoani Songwe unaounganisha Zambia na Tanzania,badala ya Bandari ya Mtwara na mpaka wa Mkenda na kwenda moja kwa moja nchini Msumbuji,hivyo kuwaongezea gharama kubwa.
Aliongeza kuwa, serikali itakapojenga barabara ya lami kutoka Likuyufusi hadi Mkenda km 124,kuna uwezekano mkubwa hata wa kujengwa kituo cha pamoja (One Stop Border Post)ambacho kitawezesha taasisi zote za serikali kuwa sehemu moja na kuwasiliana kwa haraka.
Kofi Binasi raia wa Msumbuji,ameziomba Serikali za nchi hizo kuunganisha nguvu na kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami ili kuharakisha uchumi na maendeleo ya watu wa nchi hizo.
Kwa upande wake Meneja wa wakala wa Barabara
Tanzania(TANROADS)mkoa wa Ruvuma Mhandisi Ephatar Mlavi alisema,Serikali iko mbioni kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami na hadi sasa kazi iliyofanyika ni upembuzi yakinifu.
Mlavi alisema kuwa,kwa sasa wako katika hatua za manunuzi kabla ya kumpata mkandarasi ambaye atajenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami na kumaliza kabisa changamoto ya usafiri na kufungua uchumi wa mkoa wa Ruvuma.Alisema Serikali kwa kutambua umuhimu wa eneo hilo kiuchumi, katika awamu ya kwanza itaanza kujenga km 60 za kutoka Likuyufusi hadi Muhukuru na baadaye itaendelea kujenga km 64 hadi Daraja la Mkenda linalounganisha nchi ya Tanzania na Msumbiji.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.