WANANCHI katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wameridhia kuhusu ombi la kurekebisha bei za huduma za maji lililotolewa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Songea(SOUWASA).
Wananchi hao wameridhia taftishi kuhusu ombi hilo katika kikao maalum kilichofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea kilichoshirikisha wawakilishi kutoka makundi yote wakiwemo wananchi, madiwani na wenyeviti wa mitaa.
Licha ya kuunga mkono mapendekezo ya kurekebisha bei za maji,wananchi hao wameiomba SOUWASA kuhakikisha wanaboresha miundombinu ya maji ikiwa ni Pamoja na kuongeza saa za wateja kupata maji.
“Sisi wananchi tunaunga mkono marekebisho ya bei za huduma za maji,hata hivyo tunaomba ongezeko hilo liende sanjari na kuboresha huduma zenu SOUWASA,tunapendekeza matumizi ya LUKU kwenye maji ili kupunguza malalamiko kwa wasoma mitana kuongeza mtandao wa majitaka mjini Songea,alisema Mathew Ngalimanayo,Diwani wa Kata ya mjini Manispaa ya Songea.
Akizungumza wakati anafungua na kufunga kikao hicho,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,Kanali Laban Thomas amewapongeza wananchi wa Manispaa ya Songea kwa kujitokeza kwa wingi katika kikao hicho na kuridhia mapendekezo ya kurekebisha bei za huduma za maji za SOUWASA.
RC Thomas amesisitiza kuwa maji ni huduma nyeti kwa usitawi wa wananchi na uchumi na kwamba upatikanaji wa maji safi na ya kutosha ni kielelezo cha ubora wa Maisha ya watu.
“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imekuwa ikifanya jitihada kubwa katika kufanya mabadiliko na maboresho makubwa katika sekta ya maji’’,alisema RC Thomas.
Hata hivyo amesema serikali imeongeza wawekezaji katika sekta ya maji ili kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji na kuhakikisha lengo la kutoa huduma ya maji kwa asilimia 95 mijini linatekelezwa ifikapo mwaka 2025.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa SOUWASA Mhandisi Patrick Kibasa amesema hadi sasa Mamlaka yake imefanikiwa kutoa majisafi kwa asilimia 86 na kwamba SOUWASA ina mtandao wa kusambaza majisafi wenye urefu wa kilometa 522.5 ambapo wateja 20,266 wameunganishwa katika mtandao wa majisafi.
Hata hivyo ameyataja malengo ya SOUWASA ni kuongeza upatikanaji wa maji kutoka asilimia 86 hadi kufikia asilimia 95 mwaka 2025 na kupunguza upotevu wa maji kutoka asilimia 22 hadi asilimia 20 ifikapo mwaka 2025.
Naye Mjumbe wa Bodi ya EWURA Richard Kayombo amewapongeza wadau wa Songea kutoka makundi yote kushiriki kikamilifu katika kikao hicho na kuunga mkono hoja ya kurekebisha bei za huduma za maji.
“Wananchi waliopata fursa ya kuzungumza kwenye kikao hiki shida yao sio gharama ya maji,wanachohitaji ni upatikanaji wa majisafi katika maeneo yao ili kuondoa kero ya maji’’,alisema Kayombo.
Amesema utaratibu wa kupanga bei za maji nchini,huanza kwa Mamlaka ya Maji kuwasilisha maombi yake UWURA ambapo Mamlaka inaweza kufikia uamuzi wa kuomba ongezeko la bei na tozo ili kuweza kumudu gharama zilizopanda na kuongeza mtandao wa maji kwenye maeneo ambayo hayajafikiwa.
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati (EWURA) imepewa jukumu la kudhibiti sekta ndogo ya Nishati,petroli,gesi asili na maji ambapo katika sekta ya maji na usafi wa mazingira EWURA inawajibika kudhibiti kiufundi na kiuchumi,utoaji wa huduma ya usambazaji wa maji na usafi wa mazingira.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Mkoa wa Ruvuma
Agosti 22,2022
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.