WANANCHI wa kijiji cha Chiwana na Umoja wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,wameishukuru Serikali kwa kutimiza ahadi ya kuwapatia huduma ya maji safi na salama na kumaliza tatizo la miaka mingi la wananchi hao kutumia muda mwingi na umbali mrefu kutafuta maji kwa matumizi ya kila siku.
Wametoa kauli hiyo jana mara baada ya wakala wa maji na usafi wa mazingira (Ruwasa) kukamilisha kutekeleza mradi mkubwa wa maji ambao umeanza kutoa huduma kwa wananchi hao.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake Jemshid Hamis alisema,wanawake wa kijiji hicho walikuwa waathirika wakubwa wa tatizo la maji safi na salama kutokana na kutembea umbali mrefu kutafuta maji kwa matumizi ya familia huku wakishindwa kufanya kazi nyingine za maendeleo.
Alisema, mradi huo wa maji umeleta faraja na matumaini makubwa kwa wananchi wa kijiji hicho ambapo tangu ulipoanza kufanya kazi umesaidia sana kumaliza kero ya huduma ya maji na sasa wananchi wanapata fursa ya kufanya shughuli za uzalishaji mali.
Kwa upande wake Mganga wa Zahanati ya Chiwani Jenifer Valentino alisema, kabla ya kufikishwa kwa maji safi na salama changamoto kubwa kwa wakazi wa kijiji hicho ilikuwa magonjwa ya kuhara na matumbo mara kwa mara kutokana na kutumia maji ya visima vya asili ambayo sio safi na salama.
Alisema, kwa sasa idadi ya watu wanaofika katika zahanati hiyo kutokana na kusumbuliwa na maradi hayo imepungua sana kutokana na matumizi ya maji ya bomba baada ya kukamilika kwa mradi wa maji uliotekelezwa na Ruwasa.
Hata hivyo,amewashauri wananchi wa kijiji hicho kuendelea kutumia maji ya bomba ambayo ni safi na salama kwa ajili ya matumizi yao ya kila siku, badala ya kutumia maji ya visima vya asili.
Naye Fundi Sanifu wa Ruwasa wilaya ya Tunduru Kassim Dinny alisema,mradi wa maji Chiwana ni kati ya miradi iliyotekelezwa kupitia mpango wa lipa kutokana na matokeo(P4R) kwa kuwatumia wataalam wa ndani.
Alisema,mradi maji Chiwana unahudumia vijiji viwili vya Chiwana na Umoja ambapo jumla ya wakazi wanaonufaika ni 4,281 na umegharimu jumla ya Sh. 182,531,648.88.
Alisema, kati ya fedha hizo Serikali kuu imetoa Sh.175,996,148.88,nguvu za wananchi Sh.6,535,500.00 ambapo mradi huo umetumia fedha zote zilizotengwa na Serikali,na Sh.14,036,567.72 zimeokolewa na kutumika katika kazi za nyongeza.
Kassim alitaja kazi zilizoongeza ni pamoja na kuongeza mtandao wa bomba umbali wa mita 1,265 na kufanya jumla ya mtandao wa bomba wenye urefu wa mita 4,765 na kujenga vituo vingine vinne vya kuchotea maji.
MWISHO.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.