WANANCHI wa kata ya Mahanje na Mateteleka Halmashauri ya Madaba mkoani Ruvuma,wamehimizwa kuanza ufugaji nyuki kibiashara kwa kuwa hakuna gharama katika uendeshaji wake na ina faida kubwa pamoja na soko la uhakika.
Wito huo umetolewa jana na Mkuu wa Mkoa huo Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge, wakati akizungumza na baadhi ya wakulima wa kata ya Mateteleka akiwa katika kampeni ya upandaji miti katika Jimbo la Madaba wilayani Songea.
“biashara ya ufugaji nyuki ni nzuri sana ikilinganisha na biashara nyingine kwani ukishaweka mizinga yako unasubiri nyuki waingie huku wewe unaendelea na shughuli za shamba na haulazimika kuamka asubuhi kuwatafuta nyuki na wakishaingia wanaanza kutengeneza asali ambayo unavuna mara mbili hadi tatu kwa mwaka”alisema Ibuge.
Jenerali Ibuge alisema, uzoezfu unaonyesha kuna watu wametajirika kutokana na kuuza asali ambayo ina soko la uhakika ndani na nje ya nchi tofauti na mazao mengine.
Amewataka wananchi kuchangamkia fursa ya ufugaji nyuki, kwani katika Halmashauri hiyo na kuna miti mingi inayowezesha biashara ya kufuga nyuki na kuuza asali kufanyika kwa tija, badala ya kuendelea kujikita kwenye mazao ambayo yanachangamoto nyingi ikiwamo ukosefu wa soko na bei.
Alisema,Serikali ina wajali na kuwathamini sana wananchi ndiyo maana imeanzisha utaratibu wa kutoa mikopo isiyo na riba kwa makundi ya vijana,wanawake na wenye ulemavu na kuwataka kujitokeza kuchukua mikopo ili waweze kuanzisha miradi mbalimbali ya kiuchumi.
“Ndugu zangu tumieni maeneo haya ya hifadhi kufuga nyuki,nyinyi ndiyo wanufaika na siyo mimi,jiungeni kwenye vikundi au mtu mmoja mmoja na wataalam wa TFS watawapa elimu ya namna bora ya ufugaji huo”alisema Jenerali Ibuge.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho, amewataka wakazi wa jimbo la Madaba hasa vijana kuacha kukimbilia mjini kwa ajili ya kufanya shughuli ambazo hazina manufaa ikiwamo kuendesha boda boda na kupiga debe stendi.
Amewaasa vijana,wabaki vijijini ambako kuna fursa nyingi na zenye tija kubwa kwa maisha yao na familia zao badala ya kukimbilia mjini ambako hakuna fursa zinazoweza kuwainua kiuchumi.
Alisema,ufugaji wa nyuki ni fursa mojawapo katika jimbo la Madaba na mkoa huo kwa ujumla kwani kuna maeneo yanayowezesha biashara hiyo kufanyika, na kama itatumika vizuri wananchi wataondokana na umaskini na kuchangia pato la Taifa.
Kwa upande wake Meneja wa wakala wa huduma za misitu Tanzania(TFS) Kanda ya Kusini Manyisye Mpokigwa alisema, wao kama wasimamizi wa misitu hapa nchini wako tayari kushirikiana kwa kutoa mizinga na mikopo ya fedha kwa watu walio tayari kuanza biashara hiyo.
Kwa mujibu wa Mpokigwa, TFS inaruhusu jamii kufuga nyuki katika misitu na maeneo yanayowazunguka na kuwataka wananchi kuunda vikundi vya ufugaji nyuki ili waweze kunufaika na fursa hiyo.
Alisema, ufugaji nyuki ni biashara nzuri ambayo imewaondoa watu wengi katika umaskini na bei ya asali lita 1 ni Sh. 10,000 hadi 15,000 ambapo mzinga mmoja unatoa lita 20 na kwa mwaka unavuna mara mbili.
Alisema,TFS ina mfuko maalum wa misitu ambao unatoa fedha kuanzia Sh.milioni 5 hadi milioni 50 kwa watu waliojiunga katika vikundi kwa ajili ya kuanzisha miradi ya kiuchumi ikiwamo ufugaji nyuki.
MWISHO.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.