Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amekemea tabia ya baadhi ya matajiri kuwatumikisha Watoto kwenye mashamba yao na kuathiri masomo yao.
Akizungumza na wanahabari kwenye ukumbi wa Mipango mjini Songea,Kanali Thomas amesema limeibuka tatizo la matajiri kuwatumikisha wanafunzi kwenye mashamba yao ambapo amewatahadharisha wenye tabia hiyo kuacha mara moja.
Mkuu wa Mkoa amewaagiza wakuu wote wa wilaya kuwachukuliwa hatua watu wote wanaoendelea kuwatumikisha watoto.
“Utumikishwaji wa Watoto sio tu unafanyika mashambani, imebainika katika soko kuu la Songea Watoto wanatumikishwa kuuza vifungashio muda wa jioni,nimeagiza Watoto wote watakaoonekana wanauza vifungashio wakamatwe na kuwachukulia hatua waliowajiri kufanya kazi hiyo’’,alisisitiza Mkuu wa Mkoa.
Ametoa rai kwa wanahabari kutumia vizuri kalamu zao kwa kuibua maovu yanayoendelea likiwemo la kuwatumikisha Watoto wadogo kinyume cha sheria.
Veronika Komba Mkazi wa Kijiji cha Mpitimbi wilayani Songea amekiri wamiliki wa mashamba katika Kijiji hicho kuwatumikisha wanafunzi kupanda mahindi na kuweka mbolea na kuwalipa ujira wa shilingi 5,000 na kwamba tabia ya kuwatumikisha Watoto mashambani imeshamiri pia katika Kijiji cha Mgazini na Muhukuru hivyo kuathiri masomo kwa wanafunzi.
Utumikishaji watoto wadogo bado unaendelea nchini, licha ya serikali kuweka sheria ya kumlinda mtoto mwenye umri usiozidi miaka 18.
Sheria ya haki za mtoto ya mwaka 2009, inabainisha wazi kuwa mtu hataruhusiwa kumuajiri au kumshughulisha mtoto katika aina yoyote ya kazi itakayomnyonya mtoto.
Tanzania ni miongoni mwa nchi 174 zilizoridhia Azimio la Umoja wa Mataifa namba 182 la kukomesha utumikishaji watoto chini ya umri wa miaka 18.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa amewataka wazazi na walezi ambao hawajawapeleka Watoto wao shule kuhakikisha wanawapeleka shule vinginevyo watachukuliwa hatua za kisheria.
Amesema hadi kufikia Januari 26,2024 asilimia 77.6 ya Watoto wa madarasa ya Awali walikuwa wameandikishwa,shule za msingi asilimia 91.1 na walioripoti kidato cha kwanza ni asilimia 60.9.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.