SERIKALI imetoa zaidi ya shilingi bilioni tatu kukopesha vikundi 557 vya wanawake,vijana na wenye ulemavu mkoani Ruvuma.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas wakati anazungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani ambazo kimkoa zimefanyika wilayani Mbinga.
Amesema serikali imetoa fedha hizo katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi 2023 ambapo mkopo huo umetokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri mkoani Ruvuma
“Natoa wito kwa wanawake kujiunga kwenye vikundi vyenye tija na kuanzisha shughuli za ujasiriamali ambazo zitawainua kiuchumi na kuweza kurejesha mikopo mtakayokopa “,alisema.
Ameziagiza Halmashauri zote mkoani Ruvuma kuhakikisha zinatenga asilimia kumi ya mapato ya ndani na kukopesha vikundi vya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu kila robo mwaka kama miongozo inavyoelekeza.
Akizungumzia changamoto zinazowakabili wanawake,Mkuu wa Mkoa amesema zipo changamoto zinazosababisha kuendelea kuwepo mfumo dume unaolindwa na mila na desturi potofu katika jamii.
Amewaasa wanawake kuendelea kutoa taarifa za unyanyasaji na ukatili zinapotokea pamoja na kuongeza ufahamu juu ya utambuzi wa haki na usawa kwa wote.
Risala ya wanawake wa Mkoa wa Ruvuma iliyosomwa na Joan Ngaponda kwenye maadhimisho hayo imesema maadhimisho hayo amesema mkoa una changamoto ya watoto kupata mimba za utotoni ambapo katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Desemba 2023 matukio ya mimba za utotoni yalikuwa 2,068.
Risala imetaja moja ya visababishi vya kuendelea kuwepo umasikini katika ngazi ya kaya ni wanawake kuendelea kunyimwa haki hasa umiliki wa rasikimali ardhi.
Risala hiyo imebainisha kuwa katika cha kuanzia Januari hadi Desemba 2023 mashauri 2,859 ya ukatili yalitolewa taarifa na kushughulikiwa.
Hata hivyo risala ya wanawake imeipongeza serikali kwa kusimama kidete katika kulinda haki na kujenga usawa kwa jamii tote.
Kaulimbiu ya siku ya wanawake Duniani mwaka huu ni wekeza kwa wanawake kuharakisha maendeleo ya Taifa na ustawi wa jamii.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.