WANAWAKE wakatoliki Tanzania (WAWATA)kutoka majimbo ya kanda ya kusini wameshauriwa kutimiza wajibu wao wa kulea familia zao katika misingi ya maadili ili taifa liweze kupata viongozi bora.
Ushauri huo umetolewa na Naibu Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo kuu la Songea Padre Erick Mapunda wakati akihubiri kwenye Ibada ya misa takatifu ya kongamano la wanawake wakatoliki iliyofanyika katika kanisa la Mtakatifu Mathias Kalemba mjini Songea.
Padre Mapunda amewataka wanawake hao kujitambua kuwa wao ndio nguzo na tanuli la kuwalea vijana katika misingi ya maadili kwa lengo la kukabiliana na mmomonyoko wa maadili.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Wakatoliki Kanda ya kusini Sabina Nkuba amesema kuwa katika kipindi cha siku tatu cha kongamano hilo wanawake hao wamejifunza mada mbalimbali ikiwemo juu ya kujua familia na malezi ya ndoa,wajibu wa mwanamke katika familia,kanisa na jamii.
Nkuba amezitaja mada nyingine kuwa ni wajibu wa mwanamke mkatoliki katika kujua afya ya uzazi na magonjwa ya saratani kwa akina mama,wajibu wa mwanamke katika maisha ya ndo na jinsi ya kulea utoto mtakatifu.
Katika kukabiliana na changamoto hiyo ya mmomonyoko wa maadili umoja huo wa wanawake wakatoliki umeamua kuunda umoja wa vijana na wasichana kwa lengo la kupata ndoa zilizo bora pamoja na kizazi chenye maadili.
Kwa upande wake mmoja wa washiriki wa kongamano hilo Vestina Nguruse alisema kuwa katika kipindi chote walichokuwepo kwenye kongamano hilo wameweza kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo juu ya masuala ya ujasiriamali.
Kongamano hilo limehudhuriwa na wanawake kutoka majimbo ya Mbinga,Songea,Tunduru Masasi,Njombe,Mtwara na Lindi.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Julai 10,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.