Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Ruvuma, Mheshimiwa Jacqueline Msongozi, amewasihi wanawake kuchukua hatua pindi wanapokutana na vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii.
Amesema hayo wakati akisoma hotuba kwenye kongamano la wanawake Mkoa wa Ruvuma lililofanyika katika ukumbi wa Kanisa Katoliki Bombambili mjini Songea ikiwa ni maandalizi kuelekea siku ya wanawake duniani itakayofanyika Machi 8.
“Wanawake wanakumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo ukatili wa kijinsia, nachukua nafasi hii kuwaasa wanawake kuchukua hatua mara tu tunapokutana na changamoto hii na nyingine,” alisema Msongozi.
Amewataka wakina mama wote kuwapenda na kuwa na lugha nzuri kwa watoto wao ili kuwasaidia kisaikolojia, wawe na amani na waweze kushiriki vizuri katika masomo.
Mhe. Msongozi ametaja malengo ya maadhimisho ya siku ya wanawake kwa mwaka 2025, ambapo amesema ni kuhamasisha jamii kukuza usawa, haki na uwezeshaji wa wanawake, wasichana na wanaume kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Naye Xsaveria Mlimira, akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma, amesema wamejipanga kufanya shughuli mbalimbali kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, ikiwemo kuwaona wahitaji, watoto wenye usonji waliopo Manispaa ya Songea na wakoma katika Kijiji cha Morogoro, Kata ya Litisha.
Kwa upande wake, mtoa mada ya ujasiriamali na uchumi, Dkt. Denis Mpagaze, amewashauri wanawake kufanya kazi kwa bidii ili kujipatia kipato huku akisisitiza umuhimu wa kuwa na vyanzo vya mapato vitakavyowasaidia kuendesha maisha yao bila kumtegemea yeyote.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.