Mkuu wa Wilaya Songea Mkoani Ruvuma Pololeti Mgema ametoa agizo kwa viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma kutenga fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya kutekeleza afua za lishe katika Halmashauri hiyo.
Mgema ametoa agizo katika kikao cha tathimini ya utekelezaji wa mkataba wa lishe kilicho fanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma.
Mgema ametoa agizo hilo kufuatia viashiria vya lishe kutotekelezeka kwa ufanisi katika jamii ambapo Serikali ngazi ya Mkoa hadi Watendaji wa Vijiji walisaini mkataba mwaka 2019 wa utekeleza wa afua za lishe kwa lengo la kufanikisha mapambano dhidi ya lishe duni tatizo ambalo bado lipo katika jamii.
“Ukweli ni kwamba lishe ni swala mtambuka na utapiamlo ni matokeo ya mkusanyiko wa matatizo mengi, “amesisitiza Mgema.
Mgema amefafanua kuwa Serikali inatambua umuhimu wa kuwekeza kwenye lishe kama msingi imara na mkakati wa kufanikisha shughuli za kiuchumi ambazo zitatuwezesha kufikia uchumi wa kati wa viwanda endapo tu wananchi wake watakuwa na afya bora na wenye uwezo wa kufanya kazi.
Mgema ameyataja matokeo ya lishe duni ni utapiamlo ambao unasababishwa na ulaji duni,maradhi mbalimbali,kukosa uhakika wa kupata chakula katika jamii,matunzo duni kwa mama mjamzito tangu siku ya kutunga mimba hadi kujifungua ,mazingira duni ,machafuko ya kisiasa,mgawanyo wa rasilimali usio zingatia uwiano wa kijinsia na mazingira machafu.
Mgema amezitaja baadhi ya afua za lishe ambazo zinatakiwa kutekelezwa na hazitekelezwi ipasavyo katika kupambana na tatizo la lishe duni kwenye jamii kuwa ni utapia mlo mkali,upimaji wa watoto sehemu ya juu ya mkono,utekelezaji wa vikao vya kisheria vya lishe,usimamizi shirikishi wa lishe,na utoaji wa matone ya vitamini A kwa watoto chini ya miaka mitano
Mgema ameyataja makundi ambayo yanaonekana kuathirika na tatizo la lishe duni kuwa ni Watoto chini ya miaka mitano ,wanawake walio katika umri wa kuzaa wa miaka 15-49,wanawake wajawazito ambao baadhi yao wanakabiliwa na changamoto ya kujifungua watoto njiti na wenye mtindio wa ubongo na upungufu wa damu.
Ameongeza kwa kusema takwimu zinaonyesha kuwa Halmashauri inatatizo la udumavu wa asilimia 37.4, uzito pungufu upo kwa asilimia 13, ukondondefu asilimia 18.5, uzito mkubwa kwa wanawake na wanaume ni asilimia 21.1 na upungufu wa damu kwa akinamama wenye umri wa kuzaa ni asilimia 14, na Watoto chini ya miaka mitano ni asilimia 21.
Kwa upande wake Afisa lishe wa Halmashauri hiyo Joyce Kamanga amesema lishe sasa ni swala kimaendeleo Nchini mapambano dhidi ya lishe duni ni moja ya maeneo ya kipaumbele ya miaka mitano (2016/17-2020/21); mpango wa unaolenga kutekeleza Dira yetu ya maendeleo ya mwaka 2025.
Halmashauri ya Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma inawatoto elfu 21 ambao wanatakiwa kutengewa fedha kwaajili ya utekelezaji wa afua za lishe kwenye ngazi ya Kata ambako ni kitovu cha utekelezaji wa afua hizo.
Imeandaliwa na kuandikwa na
Jacquelen Clavery
Afisa Habari Songea dc.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.