WAFANYAKAZI wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma wametekeleza maagizo ya Rais Dkt.John Magufuli kwa kufanya maombi ya kutokomeza virusi vya corona hapa nchini.
Rais Magufuli ametoa rai kwa watanzania wote kufanya maombi maalum ya kuliombea Taifa kwa siku tatu dhidi ya virusi vya corona ambavyo vinasumbua dunia nzima.
Akizungumza kabla ya maombi hayo, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma Dr.Yona Mwakabumbe amewaasa madaktari na wauguzi kufanya kazi kwa tahadhari ili kuepuka maambukizo ya corona.
Dr.Mwakabumbe amesema hospitali hiyo ipo katika hatua za mwisho za kupata mashine maalum ya kupima joto la mwili (Thermal scanner) na kwamba kuanzia Aprili 20 mwaka huu kazi ya kupima joto kwa kila mtumishi atakayekuwa anaingia katika hospitali hiyo itaanza rasmi.
Kwa upande wake Muuguzi Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Hilda Ndambalilo amepongeza kitendo kilichofanywa na wafanyakazi wa hospitali hiyo kufanya maombi maalum ya kukabiliana na corona.
Ndambalilo amesema katika janga la kukabiliana na corona, madaktari na wauguzi ni askari waliopo mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya corona na kwamba kwa kufanya maombi na kujikabidhi kwa Mwenyezi Mungu anaamini watashinda vita hiyo.
“Tutashinda kwa kishindo kikubwa katika vita hii tukijikabidhi katika maombi kwa Mwenyezi Mungu,sisi ndiyo jeshi linalotegemewa katika mapambano haya,muhimu ni kujikinga na kuchukua tahadhari,’’,alisisitiza Ndambalilo.
Dr.Mathayo Chanangula ni Daktari Msaidizi na Padre wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Ruvuma akizungumza katika maombi hayo amesema kila kitu kimeumbwa na Mungu na kwamba hata wadudu wa COVID 19 wameumbwa na Mungu na kwamba Mungu ana mamlaka ya kuwazuia na kuwatokomeza.
“ Tufanye maombi ya siku tatu kama alivyotuelekeza Rais wetu , tumuombe Mwenyezi Mungu aseme COVID 19 sasa basi,tutashinda’’,alisistiza.
Rais Dkt.John Magufuli ametoa rai kwa watanzania kufanya maombi maalum ya siku tatu kuanzia Aprili 17 hadi 19 kufanya maombi maalum ya kuliombea Taifa dhidi ya virusi vya corona ambavyo ni janga la Dunia.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Aprili 17,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.