BAADHI ya wazazi wa kata ya Mchangani Halmashauri ya wilaya Tunduru,wameishukuru Serikali kutoa Sh.milioni 66.3 ili kujenga vyumba viwili vya madarasa katika shule ya msingi Changani ambayo inakabiliwa na upungufu mkubwa wa madarasa.
Wamesema,fedha hizo zinakwenda kupunguza msongamano wa watoto wao hasa wanaosoma elimu ya awali kukaa zaidi ya 60 katika chumba kimoja cha darasa.
Said Msusa alisema,madarasa hayo yatakapokamilika yatawasaidia watoto kukaa kwa nafasi na kuongeza usikivu darasani na hivyo kufanya vizuri katika masomo yao.
Aidha alisema,ujenzi wa madarasa mapya yatahamasisha hata wanafunzi watoro kupenda kusoma kwa kuwa kutakuwa na mahali pazuri kwa ajili ya kujifunzia tofauti na sasa ambapo watoto wanalazimika kukaa dawati moja zaidi ya watatu.
Amina Mkandu,amempongeza Raid Dkt Samia Suluhu Hassan kutokana na jitihada zake za kutafuta fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ambazo zinatumika kuboresha huduma mbalimbali za kijamii.
Alisema madarasa hayo mapya ya elimu ya awali,yatahamasisha watoto kwenda shule kupata elimu na kuwataka wazazi na walezi kuhakikisha wanatumia fursa ya ujenzi wa vyumba bora vya madarasa kupeleka watoto wao shule.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Neema Lubida alisema,wamepokea kiasi cha Sh.milioni 66.3 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mawili ya elimu ya awali kupitia mradi maalum wa uboreshaji wa mazingira ya ufundishwaji kwa elimu ya awali na msingi (Boost).
Alisema,katika shule hiyo ni jumla ya watoto ni 674 wanaohitaji vyumba 15 vya madarasa,lakini yaliyopo ni 10 hivyo mradi huo utakapokamilika utasaidia kupunguza tatizo hilo.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Mchangani Hairu Mussa alisema,katika muda wa miaka miwili ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan wilaya hiyo imepokea zaidi ya Sh.bilioni 231.9 ambazo zimekwenda kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Alisema,kama Halmashauri ya wilaya wanaendelea kupambana katika suala la ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kumaliza baadhi ya changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo mbalimbali wilayani humo
Alieleza kuwa,katika shule hiyo kuna watoto zaidi ya 84 wa elimu ya awali ambao kwa sasa wanatumia chumba kimoja cha darasa,hivyo kupatikana kwa mradi huo ni faraja kubwa siyo kwa Halmashauri tu bali hata kwa wazazi na jamii nzima ya wana Tunduru.
Hairu ambaye ni mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Tunduru,amewaomba wazazi kupeleka watoto shuleni ili kupata haki yao ya msingi, badala ya kuwaacha nyumbani au kuwakimbizia mashambani.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.