WAZEE wa Mkoa wa Ruvuma wameiomba serikali kuona uwezekano wa kutoa pensheni kwa wazee wote ili waweze kukabiliana na ugumu wa Maisha.
Wazee hao wametoa ombi hilo kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas kwenye kikao cha wawakilishi wa wazee kutoka wilaya zote chenye lengo la kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili wazee kilichofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea.
Akizungumza kwenye kikao hicho Mzee Christoms Makukula ameshauri serikali kutoa pensheni kwa wazee wote kwa kuwa hivi sasa baadhi ya wazee bado wanatekeleza majukumu ya kulea wajukuu ambao wameachiwa na vijana wao.
Makukula amezitaja changamoto za wazee kuwa ni kukosa matibabu kutokana na gharama kubwa na kukosa fedha za matumizi hivyo kuishi katika mazingira magumu.
Mzee Flavina Henjewele amekemea mmomonyoko wa maadili kwa vijana ambapo amesema hivi sasa baadhi ya vijana wanatumia dawa za kulevya na kuvaa mavazi ambayo ni kinyume na mila na desturi za Mtanzania.
Mzee Yohana Mbalale amesema kutokana na changamoto nyingi zinazowakabili wazee ameshauri watumishi waliostaafu zamani waongezewe pensheni kwa kuwa fedha wanazopata ambazo ni chini ya shilingi laki moja hazitoshi kulingana na ugumu wa Maisha kwa kuwa wazee hivi sasa wanasomesha wajukuu na kuwalea.
Mbalale ameshauri kundi la wazee liwe na wawakilishi Bungeni kama ilivyo kwa watu wenye ulemavu,wanawake na vijana ili waweze kutetewa kwenye vyombo vyenye maamuzi.
Bibi Veronika Komba ameiomba serikali kutoa ulinzi wa kutosha kwa wazee ambao baadhi ya vijana wanawatuhumu kuwa ni wachawi, pia amewashauri wazazi na walezi kuwahimiza Watoto wao Kwenda makanisani na misikitini ambako watajengwa kiroho na kuepuka vitendo viovu.
Chifu wa Tano wa Kabila la Wangoni Imanuel Zulu amelitaja tatizo kubwa la vijana ni kuacha mila na desturi za Kitanzania na kuiga utamaduni wa kigeni ambapo amewataka wazazi na walezi kukemea vitendo hivyo.
Akizungumza baada ya kusikiliz kero na maoni ya wazee Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas ameahidi kufanyia kazi kero na mapendezo hayo huku akiwataka wazee hao kuwa mstari wa mbele kukabiliana na mmomonyoka wa maadili kwa vijana kwa kuwa vijana wamewazaa na wanaishi nao ambapo amesisitiza jamii nzima inahusika kukabiliana changamoto za vijana.
“Wazazi na walezi msilalamike kuhusu mmomonyoko wa maadili kwa watoto,badala yake chukueni hatua kwa sababu Watoto hao ni wenu,sote tunatakiwa kukemea maadili mabovu kwa Watoto wetu ambao ni wazazi wa kesho’’,alisisitiza.
Amesisitiza kuwa vijana wengi wamepoteza malezi na hawaendi misikini na makanisani hali inayosababisha kuacha kutenda matendo mema yanayompendeza Mwenyezi Mungu hivyo kutokuwa na hofu na Mungu
Kuhusu pensheni kwa wazee,Mkuu wa Mkoa amesema wazo hilo amelichukua na ataliwasilisha kwenye Mamlaka zinazohusika waangalia uwekezakano wa kutoa pensheni kwa wazee wote.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma anaendelea na ziara ya kusikiliza kero na maoni ya makundi mbalimbali mkoani Ruvuma hatimaye kutafutia ufumbuzi
Pichani kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas akiwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma wakisikiliza kero na maoni ya wazee wa Mkoa wa Ruvuma
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.