Na Albano Midelo,Songea
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera,Bunge na Uratibu Mheshimiwa Jenista Mhagama amezindua mradi wa kuendeleza lishe na ufugaji endelevu wa viumbe maji kwa wakulima wadogo (ARSNA) unaogharimu shilingi bilioni 3.1 katika Kijiji cha Mpitimbi wilayani Songea mkoani Ruvuma.
Waziri Mhagama amesema mradi huo unaotekelezwa na serikali katika mikoa ya Ruvuma na Lindi kwa unafadhiliwa na serikali ya Norway kupitia Shirika la NORAD na kwamba unatekelezwa kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia Machi 2024 hadi Machi 2026.
Ameutaja mradi huo kuwa umelenga kuleta mabadiliko makubwa kwenye uzalishaji na uendelezaji wa biashara ya ufugaji Samaki na uzalishaji wa mwani kwa lengo la kuwawezesha wananchi kunufaika katika maeneo yao ufugaji Samaki na uzalishaji wa mwani.
Amesema serikali imekusudia kuendeleza kilimo na uvuvi katika mikoa ya Ruvuma,Lindi ili kupata mafanikio makubwa na kuongeza tija na kukabiliana na changamoto kubwa ya upatikanaji wa vifaranga vyenye ubora na chakula cha Samaki.
“Kupitia mradi huu wazalishaji binafsi wa vifaranga vya samaki watajengewa uwezo katika uzalishaji wa vifaranga na wafugaji wa Samaki hususan vijana watajengewa uwezo wa kutengeneza chakula cha Samaki ’’,alisisitiza Mhagama.
Waziri Mhagama amesema tayari serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imejenga shamba darasa la ufugaji wa samaki katika Kijiji cha Mpitimbi ambalo amesema litakuwa chachu kubwa katika ufugaji bora wa Samaki ambapo amewaomba wananchi hao kutumia shamba darasa hilo ili kuongeza tija katika ufugaji wa Samaki.
Ametoa rai kwa wakuu wa mikoa ya Ruvuma na Lindi ambako mradi huo unakwenda kutekelezwa kuhakikisha mradi unakwenda kutekelezwa kwa ufanisi mkubwa ili kupata tija na thamani halisi ya fedha zitakazotumika.
Awali akitoa taarifa ya mradi huo Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Bunge na Uratibu Underson Mutatembwa ameutaja mradi wa ARSNA kuwa unataarajia kuzifikia kaya 5,000 za wakulima wadogo ikijumuisha wanawake asilimia 50 vijana asilimia 40 na makundi mengine asilimia 10.
Amesema mradi huo unaogharimu shilingi bilioni 3.1 unatekelezwa katika kipindi cha miaka miwili kuanzia Machi 2024 hadi Machi 2026 katika Halmashauri za Wilaya ya Songea na Mbinga mkoani Ruvuma na Halmashauri za Wilaya za Mtama na Ruangwa mkoani Lindi .
Amesema Tanzania imekuwa moja ya nchi tatu za Afrika zilizopata fursa ya kunufaika na utekelezaji wa mradi huu nchi nyingine amezitaja kuwa ni Msumbiji na Kenya na kwamba mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa program kubwa ya kuendeleza kilimo na uvuvi inayofadhiliwa na Shirika la IFAD inayotekelezwa katika mikoa 12 ya Tanzania kwa gharama ya shilingi bilioni 150.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo Mwakilishi wa Mkurugenzi IFAD Afrika Mashariki na Kusini Jacquiline Machangu amesema IFAD imekuwa ikifanya kazi na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo sekta ya kilimo hususan wakulima wadogo waliopo vijijini.
Amesema IFAD kupitia mradi wa ARSNA imelenga kuongeza mapato na kujenga uwezo kimaisha wafugaji wadogo katika maeneo matatu.
Ameyataja maeneo hayo kuwa ni ongezeko la uzalishaji na ustahimilivu kwa wafugaji wadogo wa Samaki,kuongeza kwa fursa kwa wanawake na vijana kupitia ubunifu kwenye masoko na kuendeleza ujuzi na uundaji wa sera mpya.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Alexander Mnyeti akizungumza kwenye uzinduzi huo amesema Wizara hiyo itaendelea kutoa watalaam wa uvuvi ili kufanikisha mradi huo unakwenda kuzalisha Samaki wengi kwenye mabwawa ambao wana virutubisho muhimu.
Amesema Samaki wa mabwawa wanaweza kumaliza changamoto ya udumavu kwenye Mkoa wa Ruvuma ambapo hivi sasa udumavu umefikia asilimia 37 katika Mkoa wa Ruvuma , licha ya Mkoa huo kutajwa kuwa ni ghala la chakula nchini.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed ameishukuru serikali kwa kuanza kutekeleza mradi huo mkubwa wa ufugaji Samaki katika Kijiji cha Mpitimbi.
Hata hivyo amesema serikali imekuwa inatekeleza miradi mikubwa katika jimbo la Peramiho ukiwemo mradi wa ujenzi wa barabara ya lami nzito kutoka Likuyufusi hadi Mkenda mpakani mwa Tanzania na Msumbiji.
Amesema mradi huo upo mbioni kuanza kutekelezwa serikali imetenga shilingi bilioni 74 kuanza kujenga lami kilometa 60 na kwamba serikali imetoa mabilioni ya fedha kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati mkoani Ruvuma.
Ameitaja baadhi ya miradi iliyotekelezwa kuwa ni ujenzi wa barabara ya lami nzito kilometa 66 kutoka Mbinga hadi Mbambabay kwa gharama ya shilingi bilioni 127,ujenzi wa bandari ya kimkakati ya Ndumbi kwa gharama ya Zaidi ya shilingi bilioni 12 na ukarabati wa uwanja wa ndege Songea kwa gharama ya shilingi bilioni 37.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.