WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amefungua mafunzo ya Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa mikoa na kuwataka viongozi hao waendelee kusimamia amani na utulivu kwenye mikoa yao ili watu waendelee kufanya shughuli zao bila wasiwasi wowote.
“Amani na utulivu ndiyo itatuwezesha kama nchi, tuendelee kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza mitaji yao hapa nchini. Tunakumbushwa sisi viongozi wa Tanzania tuwe wazalendo na tuhakikishe tunaziendeleza rasilimali za nchi hii kwa faida ya Watanzania wote.”
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Juni 30, 2021) wakati akifungua mafunzo ya siku nne yaliyoandaliwa na Taasisi ya Uongozi kwa lengo la kuwaimarisha viongozi ili matokeo ya uongozi wao yawapatie majawabu endelevu wananchi dhidi ya changamoto mbalimbali zinazowakabili kwenye maeneo yao. Mafunzo hayo yanafanyika jijini Dodoma.
Amesema baada ya mafunzo hayo Serikali inatarajia viongozi hao watasimamia kikamilifu nidhamu katika utumishi wa umma na kuwa kioo katika kuzingatia maadili na miiko bila kubagua jinsia, kabila, dini, rangi ya ngozi, mtu atokako ndani ya nchi ilimradi hajavunja sheria.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa mafunzo yatawawezesha viongozi hao kusimamia kikamilifu miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika ofisi zao za mikoa na za Mamlaka za Serikali za Mitaa katika maeneo yao ya utawala na kuongeza udhibiti katika ukusanyaji na matumizi ya mapato ya ndani ya halmashauri.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.