WAZIRI Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ameiagiza mikoa na Mamlaka zote za serikali za mitaa kutenga bajeti ya kuyahifadhi maeneo yote ya kihistoria ili kutopoteza historia yake kwa manufaa ya Taifa.
Majaliwa ametoa agizo hilo katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa kwenye kilele cha tamasha la kumbukizi ya miaka 114 ya vita ya Majimaji lililofanyika kwenye viwanja vya Makumbusho ya Taifa ya Majimaji mjini Songea.
Waziri Mkuu pia ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kuendelea kuadhimisha kumbukizi hizo ili ziwe sehemu ya vivutio vya utalii nchini ambazo zinachangia kuongeza pato la Taifa na kwamba Wizara hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Habari zihamasishe na kuelimisha jamii fursa za kumiliki maeneo ya malikale.
Akizungumzia mashujaa wa vita ya Majimaji ,Waziri Mkuu ameagiza kumbukumbu zilizopo ndani ya Makumbusho ya Taifa ya Majimaji zinaendelea kuhifadhiwa ili kujenga uzalendo na kuleta utaifa kwa kizazi kilichopo na kijacho.
“Mkoa wa Ruvuma hivi sasa una makumbusho mawili ambayo ni Makumbusho ya Majimaji na Makumbusho ya Dkt.Hayati Rashid Mfaume Kawawa,Mkoa huu ndiyo kitovu cha kusaidia wanaharakati wa ukombozi wa Afrika hususan nchi jirani ya Msumbiji’’,alisisitiza Waziri Mkuu.
Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Songea mjini Dkt.Damas Ndumbaro akizungumzia kumbukizi ya miaka 114 tangu kunyongwa mashujaa wa vita Majimaji,amesema maadhimisho hayo yamelenga kuenzi ushujaa wa wazee wetu katika harakati za awali za ukombozi dhidi ya wakoloni.
“Maisha ya wazee wetu ni fahari yetu kwa sababu wazee hawa walipigania nchi kwa uzalendo wa hali ya juu,ukombozi wa mwafrika una historia kubwa sana hapa kwa sababu mapambano yaliyofanyika kwa muda mrefu zaidi dhidi ya mkoloni nchini Tanzania yalifanyika Songea’’,alisema Dkt.Ndumbaro.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Christawaja Ntandu ameyataja malengo ya tamasha la kumbukizi ya mashujaa wa majimaji ambalo hufanyika kila mwaka kuwa ni kukumbuka na kuwaenzi mababu zetu ambao walinyongwa Februari 27,1906 na kuzikwa kwenye makaburi mawili ndani ya makumbusho ya Majimaji.
Hata hivyo amesema tamasha hilo hutoa fursa kwa wananchi kutunza,kuenzi na kuendeleza uzalendo,amani na mshikamo ambao umerithiwa kutoka kwa mababu zetu na kwamba tamasha hilo pi hutumika kuibua na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo ukanda wa kusini.
Naye Mkurugenzi wa Makumbusho ya Taifa Dkt.Noel Lwoga amesema wazee waliopigana katika vita ya Majimaji miaka 114 iliyopita dhidi ya wakoloni walitoa mchango mkubwa katika kutetea taifa letu na kwamba vita ya Majimaji imebeba utajiri mkubwa wa historia ya ukombozi na uhuru wa nchi yetu.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Februari 27,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.