Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Innocent Gashungwa ameziagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa maeneo yote ya kihistoria yanalindwa na kutunzwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Waziri Gashungwa ametoa agizo hilo alipotembelea eneo la hifadhi ya Makumbusho ya kihistoria ya watu wa Msumbiji lililopo Kata ya Masonya wilayani Tunduru Mkoani Ruvuma.
Amelitaja eneo la Masonya kuwa limesheni utajiri mkubwa wa historia ya Tanzania na namna Tanzania ilivyoshiriki katika harakati za ukombozi wa bara la Afrika ambapo alifurahishwa na nyumba iliyotumiwa na Rais wa zamani wa Msumbiji hayati Samora Machel kati ya mwaka 1966 hadi nchi hiyo ilipopata uhuru mwaka 1975 na nyumba iliyokuwa inatumiwa na baba wa Taifa hayati Julius Nyerere.
“Historia yote tajiri imezama katika kata ya Masonya,naziagiza Halmashauri zote nchini kutunza maeneo yote ya kihistoria,mimi nitatembelea kila Halmashauri nchi nzima ili kuhakikisha maeneo yenye utajiri wa kihistoria yanatunzwa na kuhifadhiwa’’,alisisitiza.
Awali akitoa taarifa ya eneo hilo,Katibu Tawala wa Wilaya ya Tunduru Mwajuma Abasi Nasombe alisema mwaka 1966 Tanzania iliwapokea wapigania uhuru wa Msumbiji na kuwakabidhi eneo la Masonya lililopo kilometa 16 toka Tunduru mjini.
Amesema hivi sasa eneo hilo limebaki kama eneo la makumbusho ambapo ametaja urithi unaopatikana katika eneo hilo kuwa ni nyumba mbili za viongozi wa kitaifa hayati Samora Machel Rais wa kwanza wa Msumbiji na Nyumba aliyokuwa anafikia baba wa Taifa hayati Julius Nyerere.
Nasombe ameutaja urithi mwingine kuwa ni jengo moja la mawasiliano alilokuwa anatumia Rais Samora Machael,ukumbi wa semina aliokuwa anatumia Samora Machel kutoa mafunzo mbalimbali na majengo 11 ambayo kwa sasa ni madarasa ya wanafunzi wa sekondari ya wasichana Masonya.
“Maeneo mengine ya urithi ni mahandaki yaliyotumiwa na wapigania uhuru wa Msumbiji,eneo la bendera ya FRELIMO na eneo la mnara ulipofanyika mkutano wa wanawake wa Msumbiji tarehe 17/3/1973 ‘’,alisema Nasombe.
Hata hivyo amesema mwaka 1975 baada ya nchi ya Msumbiji kupata uhuru wapigania uhuru hao walirudi katika nchi kwao na kuanzia mwaka 1990 Halmashauri ya Tunduru iliamua kuanzisha shule ya sekondari ya wasichana Masonya ambayo hadi kufikia mwaka 2014 inachukua wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha sita.
Tito Mboma ni Mwalimu wa sekondari ya wasichana Masonya na Mtaalam wa Makumbusho ya Masonya,amesema Rais wa sasa wa Msumbiji Philip Nyusi amesoma shule ya msingi FRELIMO katika eneo la Masonya na kwamba alifika hapo mwaka 1970 akiwa na umri wa miaka nane.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Februari 27,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.