Waziri wa Katiba na Sheria na Mbunge wa Jimbo la Songea mjini, Dkt. Damas Ndumbaro, amekabidhi vifaa tiba vya utengamao katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Songea (HOMSO) vyenye thamani ya shilingi milioni 10.
Katika hafla ya kukabidhi vifaa hivyo ambayo imefanyika katika Hospitali hiyo, Dkt. Ndumbaro amesema maombi ya kupata vifaa hivyo ambayo yalitolewa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Songea Dr. Magafu Majura yanakidhi vigezo vya kuchochea maendeleo ya wananchi.
"Endapo mwananchi atatibiwa haraka na kupata nafuu na kupona kabisa atarudi kwenda kufanya kazi zake za kimaendeleo na hiyo ndio tafrisi ya kuchochea maendeleo,"alisema Dkt. Ndumbaro.
Ameongeza kuwa wanufaika wa vifaa hivyo sio watu wa Jimbo la Songea mjini pekee bali ni wa majimbo yote ya mkoa wa Ruvuma hadi nchi jirani ambao wanafika kutibiwa katika hospitali hiyo kwa kuwa idara ya utengamao imekuwa ikuhudumia wagonjwa wengi.
Naye Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dr. Chihoma Mhako, ameeleza kuwa uwepo wa kitengo hicho katika hospitali ya mkoa umesaidia wagonjwa wengi ambao walikuwa wakipelekwa rufaa kwenye hospitali za kanda Mbeya au Mtwara.
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Songea, Dr. Magafu Majura ameeleza kuwa Idara ya Utengamao katika hospitali hiyo inatoa huduma ya utengenezaji na ukarabati wa viungo saidizi, matibabu ya kurekebisha na kuzuia ulemavu, huduma baada ya upasuaji wa mifupa, misuli na mishipa ya fahamu pamoja na kutoa Elimu ya kuzuia ulemavu na utengamao kwa wateja na jamii.
Amebainisha kuwa kwa mwaka 2023/24 Idara ya Utengamao imehudumia wagonjwa 7,171 ambapo ni wastani wa wagonjwa 590 kwa mwezi ambao wamekuwa na matatizo ya mgongo kwa muda mrefu, kiharusi , utindio wa ubongo, mguu kifundo, mishipa ya fahamu na maumivu mbalimbali ya viungo na misuli.
Vifaa tiba hivyo vilivyokabidhiwa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Songea (HOMSO) vimenunuliwa na fedha iliyotoka katika mfuko wa kuchochea maendeleo jimboni.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.