Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Bi. Mary Makondo amekabidhiwa vifaa tiba vyenye thamani ya milioni 10,450,000 na Taasisi ya WILOLESI Foundation vitakavyowasaidia watoto wachanga wanaozaliwa na changamoto mbalimbali katika Hospitali ya Mkoa, Songea (HOMSO).
Makondo amekabidhiwa vifaa hivyo katika hafla iliyofanyika Hospitali ya Mkoa,Songea (HOMSO) iliyopo mjini Songea, ambapo ameishukuru Taasisi hiyo kwa kufanikisha upatikanaji wa vifaa hivyo.
"Tunawashukuru na kuwapongeza sana taasisi ya WILOLESI Foundation kwa kuwa na maono na kufanikisha shughuli ya mbio za hisani zilizolenga kupata fedha za kusaidia ununuzi wa vifaa tiba kwa ajili ya kusaidia watoto waliozaliwa na changamoto mbalimbali," alisema Makondo.
Amebainisha kuwa Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya Afya ikiwemo miundombinu, rasilimali watu, dawa na vifaa tiba lakini bado wanatambua mchango wa wadau wengine kama WILOLESI Foundation katika kuunga mkono jitihada za Serikali hasa katika kuboresha afya za watoto wachanga.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dr. Louis Chomboko, amesema wanapokea vifaa hivyo vilivyotolewa na WILOLESI Foundation na vitatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Ameongeza kuwa wanaendelea kufanya juhudi mbalimbali ndani ya mkoa ili kukabiliana na changamoto zinazowapata watoto wachanga wanapozaliwa, ambapo asilimia 62 ya hospitali 18 za Mkoa mzima zinatoa huduma ya kusaidia watoto wachanga wanapopata changamoto na takribani asilimia 48 ya vituo vya afya vinavyotoa huduma ya upasuaji navyo vinasaidia watoto hao.
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa, Songea, Dr. Revocatus Makaranga, akitoa taarifa ya kitengo cha watoto wachanga kwa mgeni rasmi amesema kitengo hicho kinalaza na kuhudumia watoto takribani 80 kwa mwezi, ambao ni watoto waliozaliwa kabla ya wakati, waliopata homa ya manjano baada ya kuzaliwa na waliozaliwa baada ya miezi tisa na kupata changamoto mbalimbali za afya.
Vifaa hivyo vilivyokabidhiwa na WILOLESI Foundation ni Radiant warmer iliyogharimu shilingi milioni 5,900,000, CPAP Machine milioni 3,800,000 pamoja na Wheelchair with table laki 750,000 na kufanya jumla kuwa milioni 10,450,000.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.