Ili kupunguza hali duni ya lishe mkoani Ruvuma, Wizara ya Afya imeandaa semina maalum kwa waandishi wa habari na wadau wa lishe.
Semina hiyo imelenga kuwajengea uwezo kuhusu kanuni za uongezaji wa virutubishi kwenye chakula, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa serikali kutokomeza tatizo la lishe duni nchini.
Semina hiyo imefanyika , katika ukumbi wa Mipango wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.
Akizungumza katika semina hiyo, Daktari Luis Chomboko, aliyemwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, amesema kuwa mkoa huo ni miongoni mwa maeneo yenye hali duni ya lishe.
Tafiti za mwaka 2022 zinaonesha kuwa kiwango cha udumavu mkoani Ruvuma kimefikia asilimia 35.6.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Lishe kutoka Wizara ya Afya, Bi. Neema Joshua, amesema kuwa serikali imejipanga kutatua tatizo la lishe pungufu ili kupunguza magonjwa yanayotokana na upungufu wa lishe.
Ameeleza kuwa hatua mbalimbali zimechukuliwa, ikiwemo kuongeza virutubishi kwenye vyakula vya kila siku.
Naye Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwanangu Tanzania, Bw. Water Miya, amesema kuwa tatizo la udumavu linatokana na lishe duni, hususan upungufu wa madini na vitamini muhimu mwilini.
Amesisitiza kuwa taasisi yake inasaidia kwa kuongeza virutubishi kwenye vyakula, jambo linalosaidia kupunguza matatizo kama mtoto kujaa kichwa na mgongo wazi.
Aidha, Bw. Miya amewataka wakazi wa Ruvuma kutumia vyakula vyenye virutubishi kwa wingi, kwani licha ya kuwa mkoa unaozalisha chakula kwa wingi, bado una kiwango kikubwa cha udumavu.
Amesema kuwa ukosefu wa lishe bora kwa watoto unaweza kusababisha matatizo ya afya kama uoni hafifu na madhara ya ubongo, hivyo ni muhimu kuzingatia lishe bora kwa afya bora ya jamii.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.