Wizara ya Afya imeendesha semina kwa waandishi wa habari na wadau wa lishe mkoani Ruvuma ambayo imelenga kuwaongezea ujuzi ili waweze kufikisha ujumbe sahihi na kuielimisha jamii juu ya matumizi ya chakula kilichoongezwa virutubishi.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dr. Louis Chomboko, akifungua semina hiyo kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa, amesema baada ya semina hiyo waandishi wa habari na wadau wa lishe wanatarajiwa kuwa wahamasishaji wa kanuni za uongezaji virutubishi kwenye vyakula ili kupunguza tatizo la upungufu wa madini na vitamini katika mkoa wa Ruvuma.
Amebainisha kuwa kwa mujibu wa takwimu za afya na viashiria vya malaria za mwaka 2022, hali ya udumavu katika mkoa wa Ruvuma ni asilimia 35.6, uzito pungufu ni asilimia 12.2, upungufu wa damu kwa watoto walio chini ya miaka 5 asilimia 45 na upungufu wa damu kwa wajawazito asilimia 30.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya MWADETA (Mwanangu Development Tanzania), Walter Miya, akitoa Elimu kwa waandishi wa habari juu ya kuielimisha jamii kuhusu matumizi ya chakula kilichoongezwa virutubishi, ameyataja madhara yanayotokana na kula vyakula visivyo na madini ya Foliki ambayo ni watoto kuzaliwa wakiwa na tatizo la kichwa kujaa maji na mgongo wazi ambayo hivi sasa yanakua kwa kasi.
Ametoa wito kwa wananchi wote hususan wanawake kula chakula chenye madini ya Foliki na kutumia vidonge vya Foliki ili kuzuia kuzaa watoto wenye matatizo ya kichwa kujaa maji na mgongo wazi.
Semina hiyo imelenga kuwaongezea ujuzi waandishi wa habari na wadau wa lishe ili waweze kufikisha ujumbe sahihi na kuielimisha jamii kuhusu matumizi ya chakula kilichoongezwa virutubishi lengo likiwa ni kupunguza madhara yanayotokana na ukosefu wa madini hayo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.