SHIRIKA la kimataifa WWF limetoa elimu na vifaa kwa kukabiliana na tembo waharibifu katika vijiji vitano vilivyopo Halmashauri ya Namtumbo mkoani Ruvuma.
Akizungumza wakati anamkabidhi vifaa hivyo,Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Mhifadhi na Melimishaji wa WWF Ally Thabiti Mbugi amesema wametoa elimu ya kujikinga na wanyama waharibifu hususan tembo kwa wananchi ili kukabiliana na uharibifu bila kuleta madhara kwa wanyama.
Mbugi amesema licha ya elimu,WWF pia imetoa msaada wa vifaa mbalimbali vitakavyotumika kama nyenzo ya kukabiliana na tembo waharibifu ambapo vifaa aina ya vilipuzi 400 vimetolewa kwa wilaya ya Namtumbo.
Amevitaja vifaa vingine kuwa ni magunia ya pilipili,vilipuzi kamba na vitambaa vya pamba ambavyo vinatumika katika utengenezaji wa wigo wa pilipili ambao unasaidia kuzuia tembo wasiharibu mashamba ya wananchi.
‘’Hivi sasa tunakaribia msimu wa kilimo hivyo tumetoa elimu na vifaa mapema kabla ya uharibifu kufanyika,hata hivyo katika Mkoa wa Ruvuma tutatoa vilipuzi 800 katika wilaya za Namtumbo na Tunduru ambapo kuna uharibifu wa mazao unaofanywa na tembo,pia tumetoa mbegu za pilipili ili wananchi mwakani wasipate tabu’’,alisema.
Akizungumza mara baada ya kupokea vifaa hivyo Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Dkt.Julius Ningu amewapongeza na kuwashukuru WWF kwa msaada huo kutokana na ukweli kuwa Namtumbo imeathirika na wanyamapori waharibifu wa mazao.
‘’Ukiangalia mkulima mtaji wake ni nguvu zake mwenyewe,na anafanya kilimo cha msimu, hivyo wanyama wanapoharibu mazao ni pigo kwake’’,alisisitiza.
Amesema msaada uliotolewa na WWF serikali na wananchi wanauthamini na wataifanyia kazi iliyokusudiwa na kwamba serikali itashirikiana na wananchi kuhakikisha wanyama waharibifu wanarejeshwa kwenye maeneo yao ya asili.
Amesema ameshukuru elimu na msaada huo kutekelezwa kabla ya msimu wa kilimo hivyo inatoa nafasi kwa serikali kuwaandaa wananchi pamoja na namna ya kuvitumia vifaa vilivyoletwa ili vitumike kwa tija.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Oktoba 6,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.