JAMII nchini, imetakiwa kujenga mazoea ya kuwahusisha watoto wenye umri mdogo katika shughuli za maendeleo ikiwamo utunzaji wa mazingira na ulinzi wa rasilimali zilizopo kwa manufaa ya nchi yetu.
Wito huo umetolewa kwa nyakati tofauti na Afisa Mhifadhi wa shirika la Kimataifa la utunzaji mazingira(WWF-Tanzania) Deogratius Kilasara, wakati akizungumza na wanafunzi wa shule ya Sekondari Namwinyu na Matemanga wilayani Tunduru akiwa katika uhamasishaji wa mpango wa elimu ya uhifadhi mazingira mashuleni.
Alisema,sehemu mojawapo ya kufikisha ujumbe haraka kwa jamii nzima ni kuhusisha watoto hasa wenye umri mdogo kwani wao ndiyo wanaoshika sana wanachoambiwa au kusikia tofauti na watu wazima.
“Hawa watoto ukiwaambia kitu wanabeba hivyo kilivyo kupeleka kwa jamii,sio kama watu wazima ambao wana mambo mengi kichwani,ndiyo maana WWF kama wadau wa uhifadhi mazingira baada ya kutambua hilo tumeona ni vyema katika mpango wetu wa mwaka huu tuanze na watoto waliopo shule za msingi na sekondari”alisema Kilasara.
Alisema, katika mpango huo wanafunzi wa shule za msingi na Sekondari wataunda klabu za mazingira zitakazofahamika kwa jina la Miyombo Klabu ambapo watafundishwa namna ya kutunza mazingira,mapori na maeneo yaliyohifadhiwa ambako wanyama pori wanapatikana.
Alisema,lengo ni kutoa elimu kwa wanafunzi ili waweze kufahamu umuhimu kuhifadhi na kutunza wanyamapori ambao kama wakitunzwa vizuri Taifa litapata faida nyingi zinazotokana na utalii wa uwindaji na utalii wa picha.
Aidha alisema, elimu hiyo itawawezesha wanafunzi kushiriki moja kwa moja kusaidia katika suala zima la kutunza mazingira wakiwa katika umri mdogo na kufanikisha malengo na mipango iliyokusudiwa.
Alisema,shule zitakazohusika kwenye mpango huo zitaanzishwa bustani za miche ya miti kwa kuamini kwamba miche hiyo itasaidia kuibadilisha jamii dhidi ya vitendo vya uharibifu wa mazingira.
Kilasara alieleza kuwa,wameanza kutoa elimu na mafunzo kwa wanafunzi wa shule za msingi na Sekondari katika wilaya ya Namtumbo na Tunduru na wataendelea katika wilaya ya Liwale na Rufiji ambako WWF wanafanya shughuli zao na hadi sasa wamefanikiwa kuzifikia shule 30.
Mhifadhi wa Mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori Tanzania(Tawa) Ashura Hassan alisema,wameshatoa elimu ya kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu katika vijiji mbalimbali vinavyozunguka mapori na maeneo yaliyohifadhiwa ambapo sehemu kubwa washiriki walikuwa watu wazima.
Alisema,kwa sasa wameona ni vyema wakafika mashuleni ili wanafunzi nao waweze kufahamu umuhimu wa kutunza mazingira na kulinda rasilimali za nchi yetu kama vile wanyama na misitu katika maeneo yao ambapo TAWA inatoa elimu ya kujilinda na wanyama wakali na waharibifu hususani Tembo wanaovamia mashamba na kuharibu mazao.
Aidha,amewataka wananchi kuacha kulima ua kufanya shughuli zozote za kibinadamu kwenye maeneo ya hifadhi ili kuepuka madhara makubwa yanayoweza kutokea.
Kwa upande wake Afisa Uhusiano wa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere anayesimamia mahusiano ya ujirani mwema katika wilaya ya Tunduru Stephen Mpondo alisema, wanatoa elimu kwa jamii ili waweze kuheshimu na kutunza hifadhi zilizopo kwa faida ya jamii nzima.
Alisema,kuna sababu kubwa ya wanyama waharibifu hususani Tembo kuvamia makazi ya wananchi wanaoishi kuzunguka hifadhi hiyo na kufanya uharibifu,kula mazao na hata kujeruhi wananchi pindi wanapojaribu kuwafukuza ili warudi katika hifadhi.
Alisema, sababu mojawapo ni jamii kwenda kufanya shughuli zao ndani ya hifadhi ikiwamo kilimo na ufugaji,hivyo elimu hiyo ina lenga kuwasaidia namna bora ya kuepukana na wanyama wakali na waharibifu,pamoja na kujilinda kwa kutumia njia mbadala ikiwamo kulima mazao yasiyopendwa kuliwa na wanyama.
Mwanafunzi wa shule ya Sekondari Namwinyu Tabia Mtua alisema,elimu hiyo itawasaidia kujilinda na wanyama wakali kama Tembo ambao wanapatikana kwa wingi katika maeneo yao kutokana na kupakana na Hifadhi ya Nyerere.
Imeandikwa na Albano Midelo
wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Mkoa wa Ruvuma
Mei 17,2022
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.