Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Emmanuel Nchimbi, ametoa wito kwa wahariri na waandishi wa habari kuandika habari zinazojenga mshikamano katika taifa na sio zinazochochea chuki.
Ametoa wito huo wakati akifungua mkutano maalum wa jukwaa la wahariri Tanzania (TEF) uliofanyika katika ukumbi wa Kanisa Katoliki la Bombambili, uliopo manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
“Wahariri wa vyombo vya habari ambao ndio mnaruhusu habari yoyote itoke kwenye chombo cha habari, kama mngetumia nafasi zenu vibaya inawezekana nchi isingekuwa kama ilivyo leo, wahariri ndio chujio la habari zote katika taifa, kwa siku zote ambazo mmetimiza wajibu wenu mmefanya taifa letu kuwa na utangamano,” alisema Dkt. Nchimbi.
Dkt. Nchimbi ameeleza kuwa vyombo vya habari vinatakiwa kuhakikisha vinakemea wanasiasa wa upande wowote anayetamka mambo ambayo yanaweza kusababisha vurugu au maumivu kwa raia na hata kupelekea vifo.
Pamoja na mambo mengine katika mkutano huo, amepongeza juhudi za Jukwaa la Wahariri kwa kuendesha uchaguzi wa viongozi wake kwa misingi ya demokrasia na uwajibikaji, akisema kuwa ni mfano mzuri wa taasisi zinazoendeshwa kwa uwazi na ushirikishwaji.
Naye Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma, amesema wizara itaendelea kusimamia uhuru wa vyombo vya habari na maslahi ya wanahabari na wataendelea kushirikiana na wadau wa sekta hiyo ili kuhakikisha mazingiza bora ya uendeshaji wa vyombo vya habari nchini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amezitaja changamoto ambazo zipo katika tansnia ya habari ambazo ni uendelevu wa kiuchumi, uhuru wa wanahabari pamoja na maslahi ya waandishi wa habari.
Hata hivyo amebainisha kuwa serikali inatambua changamoto hizo na imekuwa tayari kushirikiana na jukwaa hilo ili kuzitatua, na wanaamini kwamba kwa pamoja wanaweza kubuni mbinu bora za kuhakikisha vyombo vya habari vinabaki imara na kutoa huduma bora kwa jamii.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.