Balozi wa Msumbiji nchini Tanzania Mheshimiwa Ricardo Mtumbuida ameipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kuboresha miundombinu katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma hali iliyosababisha hospitali hiyo kutoa huduma zenye viwango vya hospitali ya Rufaa.
Balozi Mtumbuida ametoa pongezi hizo katika ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Ruvuma,ambapo ametembelea na kukagua baadhi ya majengo yakiwemo jengo la wagonjwa wa dharura(EMD),jengo la wagonjwa mahututi (ICU) Pamoja na majengo ya huduma nyingine zinazoendena na hospitali ya Rufaa ya Mkoa.
Awali akitoa taarifa ya hospitali hiyo Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma Daktari Bingwa Magafu Majura alisema hospitali hiyo ilianzishwa na wakoloni mwaka 1920 ambapo awali ilikuwa ni kambi ya jeshi la Waingereza.
Amesema mwaka 1946 serikali ya waingereza iliongeza majengo mengine kwa ajili ya kutoa huduma kwa wanajeshi na familia zao na kwamba ilipewa hadhi kuwa hospitali ya wilaya mwaka 1961 na kwamba mwaka 1964 ilipandishwa hadhi kuwa hospitali ya Mkoa wa Ruvuma.
Dr.Majura anabainisha zaidi kuwa hospitali hiyo ilipewa hadhi ya kuwa hospitali ya Rufaa ya Mkoa mwaka 2009 ambapo amesema hospitali hiyo inatoa huduma zote muhimu ikiwa na vitanda 321 na watumishi 431 wa kada mbalimbali wakiwemo madaktari bingwa wanane.
Ili kuboresha huduma za afya katika Hospitali hiyo, Dr.Majura amesema serikali imetoa shilingi milioni 630 kujenga jengo la dharura (EMD) katika hospitali hiyo ambalo limeanza kutumika na kwamba serikali pia imetoa fedha kwa ajili ya wodi ya wagonjwa mahututi (ICU) yenye vitanda 12 ambayo tayari inatumika.
“Hospitali hii hivi sasa inatoa huduma mbalimbali kwa wagonjwa ndani ya Mkoa wa Ruvuma na baadhi ya wagonjwa wachache wanatoka nchi jirani ya Msumbiji’’,alisema Dr.Majura.
Akizungumza baada ya kukagua hospitali hiyo Balozi Mtumbuida amewapongeza madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo kwa kazi nzuri wanayofanya ya kuwahudumia wagonjwa ambapo amesisitiza nchi ya Msumbiji wanatakiwa kufika katika hospitali hiyo kujifunza namna huduma bora za afya zinavyotolewa.
Akiwa Mkoani Ruvuma Balozi huyo ameweza kukutana na wananchi wa Msumbiji wanaoishi mkoani Ruvuma katika wilaya za Songea,Namtumbo na Tunduru ambapo amewasisitizia serikali ya Msumbiji inafanya zoezi la usajiri wa wananchi wa Msumbiji wanaoishi nchini Tanzania hivyo wajitokeze ili kupata huduma muhimu wanazostahili kama raia wa Msumbiji.
Katika ziara hiyo Balozi huyo ametembelea Makumbusho ya Taifa ya Majimaji mjini Songea pia amekutana na uongozi wa Chama tawala CCM ngazi ya Mkoa wa Ruvuma.
Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mheshimiwa Kapenjama Ndile amemweleza Balozi huyo kuwa ,serikali mkoani Ruvuma ipo tayari kuendeleza mahusiano mazuri na nchi ya Msumbiji kwa kuendeleza ujirani mwema na jimbo la Lichinga nchini Msumbiji ambalo linapakana na wilaya ya Songea.
“Serikali mkoani Ruvuma inahimiza ujirani mwema na uhusiano mzuri baina ya Tanzania na Msumbiji kwa kuwa uhusiano huu umejengwa waasisi wa mataifa haya Mwl.Julius Nyerere na Samora Machel’’,alisisitiza Mheshimiwa Ndile.
Akizungumza kabla ya kuhitimisha ziara hiyo,Balozi huyo amesema wamefurahishwa na maendeleo makubwa yaliyofanyika katika Mkoa wa Ruvuma ikiwemo ujenzi wa miundombonu ya barabara za lami na miundombinu katika sekta za afya na elimu.
“Tanzania na Msumbiji sio nchi jirani tu bali ni ndugu wa historia ya damu kwa sababu mashujaa wengi wa Tanzania walipoteza Maisha nchini Msumbiji,pia kuna wanajeshi wa Msumbiji waliopoteza Maisha yao huku Tanzania’’,alisisitiza.
Balozi huyo ni Balozi wa Msumbiji nchini Tanzania kwa miaka miwili sasa hivyo anafanya ziara ya kujitambulisha kwenye mikoa ambayo ilitoa msaada wa hali na mali wakati wa harakati za ukombozi wa nchi ya Msumbiji.
Mikoa ambayo Balozi huyo amejitambulisha hadi sasa ni Dodoma,Iringa,Mbeya,Morogoro,Ruvuma na anatarajia kukamilisha ziara hiyo mkoani Mtwara.
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Ofisi ya Mkoa wa Ruvuma
Mei 23,2023
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.