BIASHARA ya madini ya makaa ya mawe mkoani Ruvuma imeshamiri baada ya mauzo jumla ya makaa ya mawe ya tani 450,675.32 ndani ya nchi na tani 1,060,699.05 ziliuzwa nje ya nchi katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2022.
Uchimbaji na uuzaji wa makaa ya Mawe Mkoani Ruvuma ulianza mwaka 2011 kukiwa na Kampuni moja tu ambayo ni Tancoal Energy Ltd.
Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Hamis Kamando amesema,mwaka 2019 wadau wengi walijitokeza na kufanya uwekezaji katika shughuli za Makaa ya Mawe hali iliyosababisha kuongezeka kwa uzalishaji wa madini hayo kuanzia mwaka 2020.
Amesema uzalishaji wa Madini ya Makaa ya Mawe unatoa mchango mkubwa kwenye maduhuli yanayokusanywa na Tume ya Madini Mkoani Ruvuma.
“Katika kipindi cha hivi karibuni, Makaa ya Mawe yamekuwa yakihitajika sana ulimwenguni kama chanzo cha nishati na hivyo kuwa moja ya chanzo kikubwa cha mapato ya Serikali’’,alisema Mhandisi Kamando.
Ametolea mfano,Katika Mwaka wa fedha 2021/2022, Ofisi ya Madini Mkoa wa Ruvuma ilipangiwa kukusanya maduhuli ya serikali kiasi cha Shilingi bilioni 12.
Hata hivyo amesema hadi kufikia Juni 30,2022, Ofisi ya Madini Ruvuma ilikuwa imekusanya kiasi cha Shilingi zaidi ya Bilioni 21,sawa na asilimia 179 ya lengo la Mwaka huo.
Mhandisi Kamando amesema,Katika Mwaka huu wa fedha 2022/2023, Ofisi ya Madini Ruvuma imepangiwa kukusanya zaidi ya Shilingi Bilioni 26 na kwamba hadi kufikia Desemba 31,2022,Ofisi ya Madini Ruvuma imefanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 19 sawa na asilimia 75.25 ya lengo.
“Katika makusanyo yote hayo, zaidi ya asilimia 85 yamechangiwa na uzalishaji na uuzwaji wa makaa ya mawe. Madini haya huuzwa ndani ya nchi, nchi zinazotuzunguka,barani Ulaya na Asia kupitia bandari ya Mtwara na Dar es Salaam’’,alisema..
Amesema katika Mkoa wa Ruvuma,kuna jumla ya wachimbaji 14 wanaochimba Makaa ya Mawe na kwamba katika Mwaka wa fedha 2021/2022 kiasi cha Madini ya Makaa ya Mawe kilichouzwa ni jumla ya tani 639,482.55 ziliuzwa ndani ya nchi na tani 837,846.29 ziliuzwa nje ya nchi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amesema Kwa kipindi cha hivi karibuni Mkoa wa Ruvuma umeweza kuvutia na kupata wawekezaji wengi waliowekeza kwenye shughuli zinazohusiana na madini ya Makaa ya Mawe kama Uchimbaji, Ununuzi, Usafirishaji na Uchenjuaji.
Amezitaja faida za madini ya makaa ya mawe mkoani Ruvuma kuwa ni,Kuongezeka kwa mapato ya Serikali,Kuongeza kipato kwa mtu mmoja mmoja na kupunguza utegemezi kutokana na ajira zilizopo katika uchimbaji wa Makaa ya Mawe.
Faida nyingine ni kuongeza fedha za kigeni nchini kutokana na madini hayo kuuzwa nchi za nje na Kuongezeka kwa mapato ya Halmashauri yatokanayo na ushuru wa huduma unaotozwa kwenye madini yanayochimbwa.
Shughuli za utafiti na uchimbaji wa makaa ya mawe katika mkoa wa Ruvuma zinafanyika katika Wilaya ya Mbinga maeneo ya Mbalawala,Mbuyula,Paradiso,Ntunduwaro,Amanimakoro na Ngaka, katika Wilaya ya Songea katika maeneo ya Muhukuru, Mdunduwalo,Njuga na kikunja na Wilaya ya Nyasa maeneo ya Malini.
Waziri Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa hivi karibuni ametembelea na kukagua mgodi wa makaa ya mawe wa Kampuni ya Jitegemee katika Kijiji cha Ntunduwaro wilayani Mbinga ambapo ameridhishwa kwa kushamiri kwa biashara hiyo.
Waziri Mkuu alifurahishwa na biashara ya makaa ya mawe baada ya kutembelea mgodi mmoja tu wa Jitegemee ambapo alielezwa mgodi umetoa ajira za kudumu 85,ajira za muda 150 ambapo alisema hiyo ni faida kubwa kwa wananchi na serikali ambayo inapata mapato makubwa kutokana na kodi na tozo mbalimbali.
Mkoa wa Ruvuma una hazina ya makaa ya mawe zaidi ya tani milioni 227 ambayo yanatarajiwa kuchimbwa kwa miaka 300.
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Mkoa wa Ruvuma
Januari 11,2023
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.