Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, MKOA Ruvuma Mheshimiwa Kisare Makori, amebainisha kuwa kiasi cha shilingi Bilioni 16.2 kimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa Kilomita 14.41 kutoka kata ya Utiri hadi Mahande iliyopo katika Wilaya ya Mbinga, Mkoani Ruvuma.
Amebainisha hayo wakati akisoma hotuba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed katika hafla ya makabidhiano ya mradi wa ujenzi wa barabara hiyo kwa Mkandarasi Ovans Construction Limited iliyofanyika katika kata ya Utiri Wilayani Mbinga.
"Hizi si fedha kidogo, na sisemi kwamba kazi ni ndogo, tufanye kazi usiku na mchana, mjitahidi kwa kadri mtakavyoweza wewe na timu yako ili kazi iweze kukamilika kwa wakati," alisema Mhe. Kisare.
Amemsisitiza Mkandarasi wa mradi huo kuifanya kazi hiyo kwa ubora zaidi ili mradi uweze kufanana na matarajio ya wananchi wa kata ya Utiri.
Naye Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Jumanne Mwankhoo, ametoa rai kwa wote watakaopata nafasi za kufanya kazi katika mradi huo kuwa waadilifu na kujiepusha na hujuma kwenye mradi.
Amemsisitiza Mkandarasi wa mradi huo kuhakikisha anakamilisha mradi huo ndani ya miezi 18 kama ilivyo kwenye mkataba na kwa ubora mkubwa ili thamani ya fedha iweze kuonekana na manufaa makubwa ya mradi huo yaweze kupatikana kwa wananchi.
Kwa upande wake Mkandarasi wa mradi huo Mhandisi Valence Urio amehaidi kwenda kutekeleza mradi huo kwa wakati na kwa kufuata mkataba huku akiomba ushirikiano kutoka kwa wakazi wa kata ya Utiri.
Mradi huu wa ujenzi wa barabara utakaotekelezwa na Ovans Construction Limited unatarajiwa kukamilika baada ya miezi 18.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.