KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 Abdalla Shaibu Kaim,ameweka jiwe la msingi kwenye mradi wa maji wa Ngumbo Group wilayani Nyasa unaotekelezwa na wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)kwa gharama ya Sh.bilioni 2,567,331,900.
Akitoa taarifa ya ujenzi Meneja wa Ruwasa wilayani Nyasa Mhandisi Masoud Samila alisema,mradi huo ulianza kutekelezwa rasmi mwezi Septemba 2022 baada ya taratibu za manunuzi ya Mkandarasi kukamilika na ulitarajia kukamilika mwezi Machi 2023.
Alibainisha kuwa,hata hivyo kutokana na changamoto ya mvua zilizokuwa zikinyesha kwa wingi wilayani humo Serikali ililazimika kumuongezea muda wa utekelezaji ambapo kazi hiyo itakamilika Juni 2023.
Kwa mujibu wa Samila,mradi huo utakapakamilika utakuwa na uwezo wa kuhudumia zaidi ya wananchi 11,080 wa kijiji cha Ngumbo kwa awamu ya kwanza na ya pili ambao wanatembea umbali mrefu kutafuta huduma ya maji.
Samila alitaja kazi zilizofanyika ni ujenzi wa mtego wa maji(Intake),matenki mawili ya kutunzia maji yenye ujazo wa lita 75,000 na tenki la lita 200,000,mtandao wa bomba kuu na bomba la kusambaza maji lenye urefu wa kilomita 23.18 pamoja na vituo 12 vya kuchotea maji.
Alisema,hadi sasa utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 90 na Mkandarasi kampuni ya Nipo Africa Engineering Co Ltd ameshalipwa kiasi cha Sh.milioni 385,099,785,00 ikiwa ni malipo ya awali kati ya Sh.bilioni 2,567,331,900.
Kwa upande wake Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2023 Abdalla Shaibu Kaim,ameipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kutafuta majawabu ya changamoto zinazowakabili wananchi wake.
Alisema,mradi wa maji wa Ngumbo ni matokeo ya mapenzi makubwa ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa Watanzania na kuwataka wananchi kuendelea kuiunga mkono serikali yao.
Alisema,serikali imedhamiria kutekeleza kauli yake ya kumtua mama ndoo kichwani kwa kuhakikisha inaondoa na kumaliza kabisa changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini hususani maeneo ya vijijini.
“leo wananchi wa kijiji hiki na maeneo jirani tumeshuhudia namna serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mama yetu Dkt Samia Suluhu Hassan inavyoendelea kuhakikisha suala la upatikanaji wa maji linakwenda kumalizika katika maeneo yetu”alisema.
Amewataka wakazi wa Ngumbo, kuisaidia serikali kwa kuwa walinzi wa miundombinu ili miradi inayojengwa katika maeneo yao iweze kudumu kwa muda mrefu na kuwanufaisha vizazi na vizazi.
Amewaomba kutumia fursa hiyo kuvuta maji kwenye nyumba zao kwani kufanya hivyo itapunguza msongamano wa watu kwenye vituo vya kuchotea maji(DPS) na hivyo kurahisisha suala la upatikanaji wa huduma hiyo ya maji kwenye kaya zao.
Mbunge wa Jimbo la Nyasa Mhandisi Stella Manyanya,ameishukuru serikali ya awamu ya sita kupitia Wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa),kwa kuendelea kutekeleza miradi ya maji maeneo ya vijijini na kupunguza adha ya upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.