SERIKALI kupitia wakala wa Barabara nchini(Tanroad) imetumia Sh.bilioni 37,090,185,911.00 kufanya upanuzi na ukarabati wa kiwanja cha ndege kilichopo katika eneo la Ruhuwiko Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma , kilichoanza kufanyiwa upanuzi tangu Mwezi April 2019.
Hayo yamesemwa na Kaimu Meneja wa Tanroad mkoa wa Ruvuma Mhandisi Ephatar Mlavi,wakati akizungumzia ujenzi wa uwanja huo ambapo alisema hadi sasa kazi hiyo imekamilika kwa asilimia tisini.
Mlavi alisema,kazi zilizofanywa na Mkandarasi kampuni ya Chico katika mradi huo ni kujenga barabara ya kutua na kuruka ndege,kujenga ofisi ya Mhandisi mshauri ambayo baada ya kazi kuisha itakuwa jengo la muda la abiria,kujenga maegesho ya ndege na jengo la kuweka jenereta(Power House) kazi ambazo zimeshakamilika na uwanja umeanza kutumika.
Alisema,Mkandarasi ameshalipwa jumla ya Sh.19,555,560,906.98 kwa kuwa mradi ulikamilika tangu Mei 2021 na sasa upo kwenye muda wa matazamio ambapo Mkandarasi anaendelea na kazi ndogo ndogo.
Mhandisi Mlavi alitaja kazi zilizobaki na ambazo zinazoendelea kufanyika, ni kujenga jengo la kuongozea ndege(Control Tower)ufungaji wa taa,ufungaji wa mifumo ya umeme,mifumo ya mawasiliano na ununuzi wa gari la zimamoto.
Kwa upande wake Meneja wa kiwanja cha ndege cha Songea Jordan Mchami alisema baada ya matengenezo hayo uwanja huo kwa sasa una uwezo wa kutua ndege mbalimbali ikiwamo Bombadier.
Alisema, tangu kupunuliwa kwa uwanja huo kumefungua fursa ya kiuchumi kwa wakazi wa mkoa wa Ruvuma ambapo idadi ya abiria wanatumia usafiri wa ndege imeongezeka kufuatia kupungua kwa nauli ikilinganisha kabla ya upanuzi wa uwanja huo.
Aidha Mchami, ameiomba Serikali kujenga jengo la abiria kwani lililopo ni dogo linalotosheleza kukaa abiria 50 ikilinganisha na idadi ya watu wanaofika katika kiwanja hicho kwa ajili ya kusafiri.
Amewahimiza wakazi wa mkoa huo na mikoa jirani kuendelea kutumia usafiri wa ndege ambao ni rahisi kuliko usafiri wa basi katika kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi na kuyaomba mashirika mengine kuleta ndege zao mkoani Ruvuma kwani kiwanja hicho kimekamilika na kina uwezo wa kupokea ndege aina yoyote.
Mmoja wa mkazi wa Ruhuwiko Manispaa ya Songea Jeremiha Malon, ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kuleta mradi wa upanuzi wa kiwanja cha ndege kwani umesaidia sana kuleta ajira.
Pia alisema,kuletwa kwa mradi huo kumepunguza vitendo vya uharifu hasa kwa vijana wa Songea na kuongeza idadi ya watalii wanaofika kutembelea Hifadi ya Taifa ya Nyerere na kuwaomba wananchi wa mkoa wa Ruvuma na mikoa mingine jirani ya Mtwara,Njombe kutumia kiwanja hicho kwa kusafiri kwenda maeneo mbalimbali hapa nchini.
Hata hivyo,amemuomba mkandarasi aliyepewa kazi ya upanuzi wa kiwanja hicho kukamilisha kazi zilizobaki ikiwemo kufunga taa ili kiwanja hicho kiweze kutumika hata nyakati za usiku.
MWISHO.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.