Mkuu wa Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma Mheshimiwa Kapenjama Ndile amewataka wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea kujiandaa kuupokea uwekezaji wa kiwanda kikubwa cha sukari katika Kata ya Lilai Kijiji cha Magwamila.
Ameyasema hayo wakati anazungumza katika kikao na wataalamu wa ardhi wa Halmashuri ya Wilaya ya Songea, wataalamu wa Bodi ya sukari Tanzania na wawekezaji wenyewe kutoka Madwani Group kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Songea mjini Songea.
"Tunafanya mapitio ya maombi ya wawekezaji ambapo wao wanatarajia kuweka zaidi ya bilioni 500 katika kiwanda hicho, ambapo kiwanda kitazalisha tani zaidi ya laki moja kwa mwaka’’,alisema Ndile.
Ameongeza kuwa kiwanda hicho kitaweza kuzalisha umeme ambao utaweza kuuzwa kwenye grid ya Taifa, pia kitazalisha mafuta aina ya ethane ambapo amesema kuwepo kwa kiwanda hicho kitaleta manufaa makubwa katika wilaya ya Songe ana Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla.
Kwa upande wake Mchumi Mwandamizi wa Bodi ya Sukari Tanzania Joshua Mhando amewapongeza wawekezaji kwa kuweka nia ya kuwekeza katika Wilaya ya Songea.
Hata hivyo Mchumi huyo ameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji.
Naye Mwakilishi wa Mwekezaji wa kiwanda hicho, Kapil Dave ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa kuweka utaratibu mzuri wa uwekezaji ambapo ameahidi kufanya uzalishaji wenye tija na wenye kuleta maendeleo chanya.
Eneo la uwekezaji wa kiwanda cha sukari linatarajiwa kuwa na ukubwa wa hekta 30,000 kati ya hizo hekta 22,000 zitakuwa kwa ajili ya kilimo cha miwa na hekta 8,000 kwa ajili ya ufungaji wa mitambo ya kiwanda, barabara za ndani, maghala, makazi ya watumishi, ujenzi wa huduma za kijamii.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.