HALMASHAURI NCHINI TENGENI BAJETI KWA AJILI YA WALEMAVU-NAIBU WAZIRI IKUPA
Songea
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia watu wenye ulemavu Stella Ikupa ameziagiza halmashauri nchini kutenga fedha kwenye bajeti kwa ajili ya kuwezesha shughuli za watu wenye ulemavu.
Agizo hili amelitoa leo mjini Songea wakati alipoongea na viongozi wa mkoa wa Ruvuma na halmashauri ya manispaa ya Songea akiwa kwenye ziara ya kukagua shughuli za watu wenye ulemavu.
Naibu waziri ameeleza kuwa tayari serikali ilikwisha agiza halmashauri zote kuwashirikisha watu wenye ulemavu katika kujua mahitaji yao kwa serikali,hivyo ni muhimu kutenga bajeti katika mwaka 2018/19
Akitoa taarifa ya mkoa kwa naibu waziri Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma Joel Mbewa alisema tayari halmashauri zote za Ruvuma zimetekeleza agizo la serikali kwa kutenga asilimia ya mapato ya ndani kwa ajili ya shughuli za walemavu mwaka ujao wa fedha
“Kwenye bajeti tunayoendelea kuandaa 2018/2019 mkoa wa Ruvuma umetenga asilimia kumi(10) ya mapato ya ndani kwa makundi wanawake asilimia 4,vijana asilimia 4 na walemavu asilimia 2 “ alieleza Mbewa.
Naibu waziri alipongeza na kusisitiza kuwa fedha hizi baada ya Bunge kupitisha halmashauri zihakikishe zinawafikia walengwa na kutumika kwa miradi lengwa ili ziwanufaishe walemavu wote.
“Fedha zilizotengwa kwa kundi la walemavu lazima ziratibiwe vema na kuwanufaisha wengi.Walengwa waelimishwe kuwa fedha hizi lazima zirudishwe ili wengine pia wanufaike “ alisema Ikupa
Kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mkoa wa Ruvuma kwa mwaka 2017 unakadiliwa kuwa na watu wapatao 1,542,296 ambapo watu wenye ulemavu wapo 12,972.
Taarifa ya mkoa inaonyesha mchanganuo wa wenye ulemavu na idadi yao kwenye mabano nikama ifuatavyo ; albino( 416),walemavu wa viungo (7,419),viziwi (1,527),wasioona (1,437),walemavu wa akili (1,907) na walemavu mchanganyiko (266).
Katika hatua nyingine Naibu Waziri amemwagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Tina Sekambo kuacha kununua mafuta maalum kwa watu wenye ualbino kwa gharama kubwa ya shilingi 33,000 badala yake atafute yenye unafuu ili wahitaji wengi wanufaike na huduma hii.
Mkurugenzi huyo wa Manispaa alimweleza Naibu waziri kuwa katika mwaka huu wa fedha unaoishia Juni 2018 walitenga shilingi milioni moja na nusu kwa ajili ya kununua mafuta ya wenye ualbino lakini changamoto imekuwa gharama kubwa kwenye maduka ya mjini Songea hivyo imeleta kero kwa wahitaji.
“Nia ya serikali ya awamu ya tano ni kuwafikia albino wengi kwa kuwapatia mahitaji muhimu kwa gharama nafuu .Tafuteni mafuta haya kwenye maduka nje ya Songea kwa bei nafuu ili kuokoa fedha ya serikali” alisema Naibu waziri Ikupa
Naibu Waziri Ikupa amemuomba mkuu wa wilaya ya Songea Pololet Mgema kuhakikisha kunakuwepo mkakati maalum wa kuwatambua na kuwaandikisha watoto wote wenye ulemavu shuleni.
Alitoa wito huu kufuatia taarifa ya halmashauri kuonyesha katika mwaka huu ni watoto 164 pekee wenye ulemavu wameandikishwa kujiunga na darasa la kwanza kwenye kata nane kati ya ishirini na moja za Manispaa hiyo
Naibu waziri Ikupa alisema”tunataka kila mtoto mwenye ulemavu atambuliwe na kupata haki yake ya msingi ya elimu” hivyo watumieni wenyeviti wa mitaa na vijiji kujua kaya zote zenye watoto wenye ulemavu ambao hawajapelekwa shuleni hadi sasa.
Mwisho.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.