WAKAZI wa kijiji cha Libango wilayani Namtumbo,wameishukuru serikali kutimiza ahadi yake ya kujenga na kukamilisha daraja katika mto Luegu linalounganisha kijiji hicho na maeneo mengine ya wilaya ya Namtumbo.
Wakizungumza mbele ya Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2023 Abdala Shaibu Kaim wamesema,hivi sasa kero ya kuvuka kwenye maji kila kwenda upande mwingine zimemaliza na kuhaidi kuwa walinzi wa daraja hilo ili lidumu kwa muda mrefu na liwasaidie katika shughuli mbalimbali ikiwemo usafiri na usafirishaji wa mazao.
Alisema kabla ya daraja hilo kukamilika,maisha yao yalikuwa magumu kwani walilazimika kuvuka kwenye mto huo unaojaa maji mengi hasa nyakati za masika kufika katika maeneo mengine ili kupata baadhi ya huduma za kijamii ikiwemo za afya.
Abdala Hamis,ameupongeza wakala wa barabara za mijini na vijiji(Tarura) kwa kazi nzuri iliyofanya kukamilisha daraja hilo ambalo linakwenda kuchochea uchumi wao uliodhorota baada ya daraja la zamani kusombwa na maji miaka miwili iliyopita.
Mkazi mwingine wa kijiji hicho Rashid Tapa alisema,hapo awali walilazimika kuvuka katika daraja la miti ambalo halikuwa imara kwani hata magari yalishindwa kupita na hivyo kulazimika kuuza mazao yao kwa bei ya hasara yakiwa bado shambani.
Aidha,ameiomba Tarura kufanya matengenezo makubwa ya barabara inayoanzia Libango hadi Namtumbo mjini ambayo kwa sasa imeharibika vibaya kutokana na mvua za masika zinazoendelea kunyesha kwa wingi wilayani humo.
Kwa upande wake Kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru mwaka 2023 Abdala Shaibu Kaim,amewataka wananchi hao kulinda daraja hilo kwa kutoiba vifaa vilivyotumika katika ujenzi, alama za barabara na kuepuka kufanya shughuli zozote za kibindamu ikiwemo kilimo ndani ya mita 60.
Alisema,serikali imetumia gharama kubwa kujenga daraja la Libango ili kuwasaidia wananchi waweze kufanya shughuli zao za uzalishaji mali pamoja na usafiri na usafirishaji wa mazao kutoka shambani kwenda sokoni.
Naye meneja wa wakala wa barabara za mijini na vijijini(Tarura)wilayani Namtumbo Mhandisi Fabian Lugalaba alisema,ujenzi wa daraja la Libango unatekelezwa kwa awamu kupitia fedha za jimbo na tozo ya mafuta ambapo awamu ya kwanza ilianza mwezi Septemba 2021 na kukamilika mwezi Juni 2022.
Lugalaba alieleza kuwa,katika awamu ya pili ya utekelezaji ulianza mwezi Agosti na kukamilika mwezi Disemba mwaka 2022 na awamu ya tatu itafanyika katika mwaka wa fedha 2023/2024.
Alisema,lengo la kujenga mradi huo ni kutatua changamoto ya kivuko katika mto Luegu na kuimarisha usafiri na usalama wa watumiaji wa barabara kati ya makao makuu ya wilaya,kitongoji cha Minazini na kijiji cha Libango kata ya Namtumbo ili kuboresha shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wananchi.
Aliongeza kuwa,awamu ya kwanza ya utekelezaji ilifanywa na mkandarasi M/S Jambela Ltd ambayo ilihusisha ujenzi wa daraja la mita 300 kwa gharama ya Sh.milioni 638,921,000 kupitia fedha za jimbo Sh.milioni 500 na fedha za tozo Sh. milioni 138,921.000.
Kwa mujibu wa Lugalaba,awamu ya pili imefanywa na mkandarasi M/S Sinai Ltd kwa gharama ya Sh.milioni267,509,000 kupitia fedha za tozo ambayo ilihusisha kujaza kifusi kwenye kingo za daraja,kuinua tuta la barabara na kuimarisha kingo za daraja upande wa juu wa maingilio ya mto.
Aidha alieleza kuwa,katika awamu ya tatu na ya mwisho itakayohusisha kuimarisha kingo za daraja,ujenzi wa box culvert na kuongeza ukubwa wa tuta la barabara inatarajiwa kufanyika mwaka wa fedha 2023/2024 ambapo jumla ya Sh.milioni 300 zimeombwa kupitia fedha za jimbo.
Alisema,daraja hilo limejengwa kwa kuzingatia viwango vilivyopo kwenye mkataba kati ya Serikali na mkandarasi na hadi litakapokamilika litagharimu kiasi cha Sh.bilioni 1,206,
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.