Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, leo tarehe 25 Juni 2025, amemuapisha rasmi Denis Gelvas Masanja kuwa Mkuu mpya wa Wilaya ya Tunduru akichukua nafasi ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Simon Chacha.
Hafla ya kuapishwa kwa kiongozi huyo imefanyika katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, mjini Songea.
Akizungumza baada ya tukio hilo, Kanali Ahmed amemtaka Mhe. Masanja kuhakikisha anaenda kudumisha amani, ustawi wa wananchi na utawala wa sheria, pamoja na kushughulikia haraka kero zinazowakabili wananchi.
"Ninakusihi uende ukaimarishe amani, ustawi wa wananchi na utawala wa sheria, hakikisha kero za wananchi zinatatuliwa kwa haraka na kwa ufanisi kwa kushirikiana na viongozi wenzako, kasimamie vizuri ukusanyaji na matumizi ya mapato kwa kuzingatia malengo yaliyokusudiwa, pigana na rushwa, uzembe na ufujaji wa mali za umma, na kasimamie utekelezaji wa ajenda ya maendeleo ya Mhe. Rais Dkt. Samia kwa weledi na kasi kubwa," alisema Kanali Ahmed.
Vilevile, Kanali Ahmed ametoa wito kwa viongozi wa taasisi mbalimbali za umma na binafsi, pamoja na wananchi wa Tunduru kushirikiana kwa karibu na kiongozi huyo mpya, akisisitiza kuwa ushirikiano ni msingi wa mafanikio ya kweli katika uongozi.
Kwa upande wake, Mhe. Denis Gelvas Masanja ametoa shukrani zake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kumuamini na kumpa jukumu hilo akiomba ushirikiano na watumishi wote wa Mkoa wa Ruvuma katika kuhakikisha utekelezaji wa majukumu yake unakuwa wa ufanisi na wenye tija kwa wananchi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.