MKUU wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma Mheshimiwa Ngollo Ng’waniduhu Malenya amewataka walimu wilayani Namtumbo kusimamia maadili katika shule zao ili kudhibiti mmomonyoko wa maadili ambao unajitokeza hivi sasa.
Mheshimiwa Malenya aliyasema hayo kwenye kikao kilichowashirikisha waratibu elimu kata,walimu wakuu,maafisa idara ya elimu,afisa tume ya utumishi wa walimu( TSC) na afisa kutoka ofisi ya mkaguzi na mdhibiti ubora wa shule.
Aidha Malenya amesema mmomonyoko wa maadili hivi sasa unazidi kuongezeka na kuwataka walimu hao kusimamia kudhibiti umomonyoko wa maadili kwa kutoruhusu kufanyika mapenzi mashuleni kati ya walimu wa kiume na wanafunzi wa kike lakini pia walimu wa kike na wanafunzi wa kiume,lakini pia wanafunzi kwa wanafunzi .
Hata hivyo Malenya alifafanua kuwa yeye ni mpenda mabadiliko yaliyochanya ,mpenda ukweli na mpenda usafi ,na kuwaomba walimu na viongozi wote wa wilaya ya Namtumbo kufanyakazi kama timu kwa kushirikiana kwa dhati ili kuwa na taswira ya ushindi katika mambo yanayofanyika wilayani humo.
Lakini pia mkuu wa wilaya huyo aliahidi walimu kwenda kuzungumza na wananchi kila kata wilayani humo kuhimiza swala la wanafunzi kupata chakula shuleni ili kuwasaidia wanafunzi hao waweze kujikita zaidi katika masomo badala ya kutembea umbali mrefu kufuata chakula na wakati mwingine kutopata chakula kabisa.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo Chiriku Hamis Chilumba pamoja na mambo mengine alimwambia mkuu wa wilaya kuwa halmashauri ya wilaya ya Namtumbo ina jumla ya walimu 882 huku mahitaji ni walimu 1351 ambapo sasa kuna upungufu wa walimu 469 .
Afisa elimu Msingi wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo Juma Fulluge aliagiza walimu wakuu kusimamia taaluma mashuleni kwa kuhakikisha walimu wanafundisha ipasavyo na kwa kumaliza mada zilizopo .
Fulluge alisisitiza kuwa ofisi yake itakuwa inafuatilia ufundishaji katika kila shule,ufanyikaji wa mitihani ya mihula,ufanyikaji wa majaribio ya kila mwezi na utoaji wa mazoezi kwa wanafunzi na kukazia ufundishaji kwa vipindi vya ziada kwa wanafunzi wa darasa la nne na la saba.
Mustapha Ponera mwalimu mkuu wa shule ya msingi Namtumbo akizungumza kwa niaba ya walimu wakuu wenzake alisema wao kama walimu wakuu wanaenda kusimamia taaluma ipasavyo na kuwahakikishia viongozi wa wilaya ya Namtumbo kuwa yale yote yaliyosisitizwa na viongozi hao yanaenda kufanyiwa kazi na matokeo chanya yatapatikana alisema mwalimu huyo.
Kikao cha walimu wakuu,waratibu elimu kata na maafisa wilayani Namtumbo kilifanyika jana katika ukumbi wa Halmashauri ambapo lengo la kikao hicho kilikuwa kuwahimiza kusimamia majukumu yao ya kila siku kwa kuwasisitiza walimu kufundisha madarasani pamoja na ugawaji wa vishikwambi 21 kwa waratibu elimu kata kwa kata21 zilizopo wilayani Namtumbo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.