MKUU wa Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Ngolo Malenya, amewapongeza walimu wa wilaya hiyo kwa juhudi zao katika kusimamia na kutekeleza ujenzi wa miundombinu ya shule za msingi na sekondari.
Akizungumza jana wakati wa kufungua mkutano mkuu wa uchaguzi wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Namtumbo uliofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Dkt. Samia Suluhu Hassan, Malenya alisisitiza kuwa walimu ni wadau muhimu wa maendeleo katika sekta ya elimu na jamii kwa ujumla.
Malenya alibainisha kuwa walimu siyo tu wanawajibika katika kuwajengea wanafunzi msingi mzuri wa elimu, bali pia wanashiriki moja kwa moja katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayopelekwa kwenye shule zao.
Hata hivyo, aliwataka walimu kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa weledi na kwamba Serikali haitasita kuwachukulia hatua wale watakaoshindwa kusimamia ujenzi wa miundombinu ya shule au kwenda kinyume na maadili ya kazi yao.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya aliwaagiza maafisa elimu wa shule za msingi na sekondari kuhakikisha wanazingatia sheria na taratibu wanapohamisha watumishi kutoka kituo kimoja cha kazi kwenda kingine. Alisisitiza kuwa ni muhimu kuhakikisha watumishi wanalipwa stahiki zao kikamilifu ili kuepusha usumbufu unaoweza kutokea.
Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Walimu Wilaya ya Namtumbo, Deograsias Haule, alisema chama hicho kina wanachama 1,292 ambapo 1,265 kati yao sawa na asilimia 98 ni wanachama hai. Alieleza kuwa matarajio yao ni kuhakikisha walimu wote wanajiunga na chama hicho.
Haule pia alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupewa dhamana ya kupeperusha bendera ya Chama cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu ujao, akisisitiza kuwa walimu wanatambua juhudi za serikali katika kuboresha sekta ya elimu.
Katika uchaguzi wa chama hicho, Mwalimu Jacob Mbunda alichaguliwa kuwa mwenyekiti mpya baada ya kupata kura 66 na kumbwaga aliyekuwa mwenyekiti wa zamani, Anna Mbawala, aliyepata kura 35. Uchaguzi huo ni sehemu ya mchakato wa kuimarisha uongozi wa chama katika ngazi ya wilaya kwa miaka mitano ijayo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.