Mikoa ya nyanda za juu kusini, utafitI unaonyesha ndiyo inayoongoza kuwa na kiwango kikubwa cha watoto wenye udumavu na utapiamlo.
Kauli hiyo imebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Kamando Mgema akiwa katika kikao cha tathimini ya Lishe Manispaa ya Songea kilichohudhuriwa na maafisa wa Watendaji Kata 21 na wataalamu wa afya kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Songea jana tarehe 15 aprili 2021.
Pololet alisema lengo la kuweka tathimini katika kila robo moja ya mwaka ni kuweka mkakati na mpango kazi wa lishe bora kwa jamii ili kuhakikisha tunapunguza au kuondoa kabisa tatizo la watoto wenye udumavu na utapiamlo Mkoani Ruvuma hasa Songea Mjini.
Aliongeza kuwa nyenzo muhimu ya kutekeleza mkakati wa lishe Manispaa ya Songea ni kutoa elimu kwa jamii ili kuondoa changamoto zinazojitokeza za ongezeko la watoto wenye udumavu na utapiamlo kwa watoto walio chini ya miaka mitano 5 kutoka asilimia 0.08% septemba 2020 hadi asilimia 0.16% januari hadi machi ikiwa ni ongezeko kubwa kuliko kipindi cha nyuma.
Alisema ongezeko hilo linatokana baadhi ya akimama wajawazito kutohudhuria kliniki kwa wakati, wahudumu wa afya na watendaji wa kata na Mitaa kutotembelea kaya zenye wajawazito na watoto walio chini ya miaka mitano 5, ukosefu wa elimu ya Lishe kwa Maafisa watendaji wa kata na Mitaa, pamoja na kukosekana kwa sheria ndogo ndogo za mkataba wa lishe kwa watoto walio chini ya miaka mitano 5.
Pololet amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa Songea Tina Sekambo kuwawezesha Maafisa wa watendaji wa kata kupata elimu ya mafunzo ya Lishe ili waweze kutoa elimu sahihi ya lishe kwa jamii, pamoja na uandaaji wa taarifa zenye takwimu sahihi, uwajibikaji wa kazi na uwazi wa utawala bora katika maeneo yao ya kazi kwa kubandika taarifa za kiutendaji katika mbao za matangazo pamoja na kuzingatia kanuni ya uendeshaji wa vikao vya kisheria ifikapo kila robo moja ya mwaka na uandaaji wa sheria ndogo za lishe.” Alisisitiza” .
Naye Afisa Lishe Manispaa ya Songea Florentine Joseph Kissaka alisema jumla ya watoto wenye utapiamlo mkali waliopewa rufaa kwenda kwenye matibabu ni 29 ambao walitoka kata za matarawe 1, misufini 1, matogoro 21, Ruhuwiko 1, na Msamala 5 kati ya watoto 17,840 waliopimwa sawa na asilimia 0.16 ya wenye utapiamlo katika kipindi cha januari-machi.
Kissaka alibainisha kuwa jumla ya vijiji vilivyofanya mkutano siku ya afya na lishe ni 91 kati vijiji 95 sawa na asilimia 95.8% ya utekelezaji wa zoezi hilo. Aliongeza kuwa vijiji vyenye sheria ndogo za lishe ni 77 kati ya vijiji 95 sawa na asilimia 81.1%, vijiji vilivyobandika taarifa ni 86 kati ya vijiji 95 sawa na 90.5%.
Miongoni mwa mikakati iliyowekwa ili kukabiliana na ongezeko la watoto wenye udumavu na utapiamlo Manispaa ya Songea ni pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa jamii namna ya uandaaji wa chakula cha lishe kwa mtoto chini ya miaka mitano, mpangilio wa ulaji wa chakula, na aina ya chakula kinachofaa kuliwa.
Imeandikwa na Amina Pilly
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.