MKUU wa Wilaya ya Songea Mheshimiwa Kapenjama Ndile amewataka Watendaji wa Kata na Vijiji kwa kushirikiana na Walimu wakuu wa shule kuendelea kuhamasisha Wazazi juu ya uchangiaji wa chakula mashuleni.
Ameyasema hayo wakati wa kikao cha utekelezaji wa tathmini ya Afua na Mkataba wa Lishe kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano Lundusi- Peramiho na kuudhuriwa na kamati ya Lishe ya Halmashauri ya Wilaya ya Songea.
Aidha, DC Ndile katika kikao hicho amewasisitiza Watendaji wa Kata waje na mtizamo mpya wa kutoa taarifa za utekelezaji wa Afua za Lishe kwa uharaka na ziwe sahihi.
“Naendelea kuwasisitiza Watendaji jitahidini sana kuwahisha taarifa, jambo lingine nawaomba Maafisa Elimu muwahamasishe walimu wakuu kuongea na wazazi wa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ili waweze kuchangia chakula mashuleni na kuhakikisha kila mwanafunzi anapata chakula akiwa shuleni”, amesema DC Ndile.
Akizungumza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Ndugu Neema Maghembe amesema katika kipindi cha robo ya tatu mwaka wa fedha 2022/2023 Halmashauri imefanya shughuli za usimamizi elekezi ambazo ni kuangalia utoaji wa Elimu ya Lishe katika Vituo vya kutolea Huduma za Afya, Utambuzi na matibabu ya Utapiamlo mkali na upimaji wa hali ya Lishe kwa Watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
“Sisi Halmashauri ya Wilaya ya Songea katika kutii agizo la Serikali la kutekeleza Afua za Lishe tumekuwa na mwelekeo chanya wa kutoa fedha za kutekeleza shughuli za Lishe kwa wakati ili kuhakikisha shughuli hizi zinaenda vizuri”, amesema Ndugu Neema.
Akisoma taarifa ya utekelezaji Afisa Lishe Wilaya Joyce Kamanga amesema katika robo ya tatu Watoto waliogundulika na Utapiamlo mkali walikuwa 18 kati ya hao Watoto wote wamepona baada ya kupatiwa matibabu.
Vilevile amesema Halmashauri imejipanga vizuri katika suala la kuimarisha usimamizi, pia katika kushirikisha kamati za Kata na Vijiji na wataalamu walioko katika ngazi ya Kata kwenye suala zima la kusimamia maadhimisho ya siku ya afya na lishe ambapo Wataalamu wanatoa Elimu kwa wazazi juu ya maandalizi ya Lishe na Watoto wanapata nafasi ya kupima hali ya Lishe katika Vijiji.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.