Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme ameipongeza Halmashauri ya Madaba wilayani Songea kwa kupata hati safi kwa miaka mitatu mfululizo.
Mndeme ametoa pongezi hizo wakati anafungua kikao maalum cha Baraza la madiwani la Halmashauri hiyo cha kujadili taarifa ya hoja na mapendekezo ya CAG kwa mwaka 2018/2019 kilichofanyika kwenye ukumbi wa shule ya sekondari ya Madaba.
Taarifa ya CAG imeripoti kuwa Halmashauri ya Madaba imepata hati safi kuanzia mwaka wa fedha 2016/2017 hadi 2018/2019,ambapo Mndeme amesema kupata hati safi katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo ni jambo la la kutiliwa mfano.
Mkuu wa Mkoa pia ameipongeza Halmashauri hiyo kwa kuchangia kwa asilimia 81.67 mfuko wa wanawake,vijana na wenye ulemavu kwa kuchangia shilingi milioni 32 katika bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019 na kukusanya zaidi ya shilingi milioni 578 sawa na asilimia 70.13.
Ili kuhakikisha kuwa Halmashauri hiyo inaendelea kupata hati safi,Mkuu wa Mkoa ameagiza kuzuia hoja za aina ile ile zinazojirudia mwaka hadi mwaka na wataalam kuendelea kutoa ushirikiano wakati wa ukaguzi.
“Hakikisheni mnadhibiti upotevu wa mapato katika Halmashauri na vyanzo vya mapato vidhibitiwe kwa kuchukua hatua stahiki,hakikisheni wanaodaiwa wote kupitia mashine za kukusanya mapato POS wanalipa madeni yao mara moja’’,alisisitiza Mndeme.
Katika hatua nyingine Mndeme amewaagiza wataalamu wa afya katika Halmashauri hiyo, kuhamasisha wakulima kuongeza uzalishaji wa zao la tangawizi na kujenga viwanda vya kusindika zao hilo.
Utafiti umebaini kuwa Halmashauri ya Madaba ina eneo lenye ukubwa wa hekari 888 zinazofaa kwa kilimo cha tangawizi ambapo hadi sasa wakulima wanaolima zao la tangawizi ni 256 tu ambapo Mndeme ameomba zao hilo lipewe kipaumbele kwa kuongeza kasi ya uzalishaji wake.
Mndeme ameshauri kuongeza kasi ya uzalishaji wa zao la tangawizi kutoka malengo ya uzalishaji wa zao hilo kwa mwaka 2019/2020 ya kuvuna tani 7511 kutoka hekari 288 ambapo amesema hayo ni malengo ya chini kwa kuwa soko la zao hilo ni kubwa ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Madaba Festus Mfikwa amemhakikishia Mkuu wa Mkoa kutekeleza maagizo yote aliyotatoa ili Halmashauri hiyo iendelee kupata hati safi kila mwaka na kuinua uchumi kwa kuongeza uzalishaji wa zao la tangawizi na mazao mengine kama mahindi na mapalachichi.
Mfikwa amesema Halmashauri ya Madaba inapata maendeleo kutokana na ushirikiano na umoja uliopo baina ya madiwani na watalaam.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari wa Mkoa wa Ruvuma
Juni 6,2020
Madaba
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.