OFISA Maliasili wa Halmashauri ya Nyasa Mkoani Ruvuma Bugingo Bugingo amesema hekari moja ya miti ya mitiki inaweza kumuingizia mkulima zaidi ya milioni 400.
Bugingo amesema Halmashauri ya Nyasa inatekeleza mradi wa panda miti kibiashara ikiwa imeweka lengo la Kupanda miti hekari 1750 ambapo hadi sasa miti hekari 317.5 imepandwa na inaendelea vizuri.
Hata hivyo wakulima wengi mwambao mwa ziwa Nyasa wanakata tamaa ya kupanda miti hiyo ambayo tangu kupandwa hadi kuvunwa inachukuwa kati ya miaka 15 hadi 20.
Mradi wa Pandamiti kibiashara unatekelezwa katika safu ya Milima ya Livingstone,Kata za Lipingo, Liuli, na Kihagara Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma unaendelea kwa kiwango cha kuridhisha.
Mratibu wa Mradi wa Forvac Mkoa wa Ruvuma Marcel Mtunda ,akikagua mradi wa panda miti kibiashara unaotekelezwa katika kijiji cha Mkali A na Kijiji cha Nkalachi Kata ya Liuli, ameridhishwa na maendeleo ya ukuaji wa miti, na kuwaomba wananchi wapalilie miti hiyo, ili isiungue na moto.
Amesema wananchi mara baada ya kupata elimu ya upandaji miti kibiashara, wamehamasika na kupanda miti ambapo amesema mradi huo utawanufaisha wakulima wa Miti katika vijiji hivyo kwa kuinua hali ya maisha na kuongeza kipato katika ngazi ya Familia.
Ben Mfungo ni Rais wa Shirikisho la Viwanda vya Misitu Tanzania (SHIVIMITA) tangu mwaka 1988,anabainisha mahitaji ya soko la miti aina ya mitiki ni kubwa ndani na nje ya nchi.
“Juzi tu nilikuwa Accra nchini Ghana ,tulijulishwa kwamba Jumuiya ya ECOWAS ilichukua mbegu za miti ya mitiki toka Tanzania baada ya kubainika mbegu za Tanzania zina ubora zaidi katika soko la dunia hivyo nao wameamua kuchukua mbegu hiyo inayokidhi soko la kimataifa’’,anasisitiza Mfungo.
Anawaasa wakulima wapya wa mitiki katika wilaya ya Nyasa na maeneo mengine ambayo zao hilo linaweza kustawi, waongeze uzalishaji wa zao la mitiki kwa sababu tangu enzi hizo hadi leo mahitaji yake yanaendelea kuongezeka.
Anayataja miongoni mwa matumizi ya zao la mitiki kuwa ni kutengenezea vitako vya silaha aina ya bunduki,vyombo vya majini kama vile meli na boti, na kwamba ujenzi wa mahakama kubwa duniani imetumika miti aina ya mitiki kwa sababu ndiyo mti mgumu ambao unaweza kuishi majini na nchi kavu,pia hutumika kutengeneza samani mbalimbali zenye gharama kubwa.
“Mahitaji ya mti huu katika soko la duniani ni makubwa ,ndiyo maana nchi za Ulaya na nchi za Asia zikiongozwa na China na India wananunua miti aina ya mitiki kwa wingi kutoka Tanzania,na hata hatujaweza kufikisha hata robo ya mahitaji yao’’,anasisitiza Mfungo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wiaya ya Nyasa Jimson Mhagama ametoa rai kwa wananchi, na kampuni za wawekezaji wanaohitaji kuwekeza katika sekta ya Misitu wafikie katika Wilayani Nyasa kuwekeza kwenye ardhi yenye rutuba ya kutosha .
Katika mkoa wa Ruvuma mradi huo uliofadhiliwa na nchi ya Finland unafanyika katika Halmashauri za Wilaya ya Nyasa,Mbinga na Madaba wilayani Songea.
Mshauri wa Misitu katika Mradi wa Panda Miti Kibiashara Sangito Sumari anasema katika wilaya ya Nyasa mradi huu unahusu miti aina ya mitiki ambayo utafiti umebaini inastawi vizuri katika hali ya hewa iliyopo mwambao mwa ziwa Nyasa.
Imeandikwa na Albano midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Julai 13,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.