HOSPITALI ya Halmashauri ya Wilaya Songea mkoani Ruvuma ambayo imejengwa katika kijiji cha Mpitimbi B kwa gharama ya shilingi bilioni 1.8 inatarajia kuanza kutoa huduma za matibabu kuanzia Julai 15 mwaka huu.
Akitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa hospitali hiyo kwa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Ruvuma katika eneo la mradi,Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Simon Bulunganija amesema mradi huo umefikia asilimia 95 ya utekelezaji ambapo amezitaja huduma ambazo zitaanza kutolewa na hospitali hiyo ni za wagonjwa wa nje (OPD).
Amesema ujenzi wa hospitali hiyo ulianza mwaka 2019 na kwamba katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huo Halmashauri ilipokea shilingi bilioni 1.5 ambazo zilijenga hadi katika hatua ya ukamilishaji.
“Nachukua fursa hii kwa niaba ya wananchi wa Halmashauri ya Songea kumshukuru Rais Dkt.John Magufuli kwa kutuongeza shilingi milioni 300 na kufanya mradi kutumia sh.bilioni 1.8 kutekeleza mradi huu’’,alisema Bulunganija.
Hata hivyo amesema hadi sasa zimetumika zaidi ya shilingi bilioni 1.5 na kwamba wanatarajia majengo yote saba ya hospitali hiyo kukamilika Julai 30 mwaka huu na kuwezesha huduma zote za afya kuanza kutolewa katika hospitali hiyo.
Amesema hospitali hiyo inatarajia kuhudumia kata zote za Halmashauri ya Wila ya Songea ,hata hivyo amezitaja changamoto zilizopo katika mradi huo ni mgawo wa maji ambao husababisha mafundi kukwama kukamilisha ujenzi wa hospitali hiyo kwa wakati.
Ameyataja majengo ya hospitali hiyo yanayoendelea kukamlishwa kuwa ni jengo la utawala ambalo limefikia asilimia 90,jengo la wagonjwa wa nje asilimia 80,stoo ya dawa asilimia 92,ujenzi wa maabara asilimia 92,jengo la vipimo vya mionzi asilimia 85,jengo la kufulia asilimia 90 na jengo la wazazi asilimia 90.
Akizungumza mara baada ya ukaguzi wa hospitali hiyo,Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho ameupongeza uongozi wa Halmashauri hiyo kwa kutekeleza mradi huo,hata hivyo amewaomba kuongeza kasi ili wananchi waanze kupata huduma hiyo.
“Sisi tunakimbizana na muda mwaka 2015 tuliwaahidi wananchi kwamba tutawasogezea huduma ya afya jirani hivyo tunataka wananchi waanze kupata huduma zote ili wakati wa Kampeni tuwaambie wananchi tuliahidi tumetekeleza’’,alisisitiza Mwisho.
Katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa maji,Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini RUWASA katika Wilaya ya Songea Mhandisi Samwel Sanya amesema wanatarajia kupeleka huduma ya maji katika hospitali hiyo ifikapo Julai 30 mwaka huu.
Naye Mbunge wa Jimbo la Peramiho Jenista Mhagama ameutaja mpango wa muda mrefu wa kukabiliana na upungufu wa maji katika eneo la hospitali na wakazi wa kijiji cha Mpitimbi ni kuchimba visima virefu na kwamba fedha za kutekeleza mradi huo katika jimbo zima la Peramiho zimekwishapokelewa.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Julai 7,2020
Songea
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.