Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma iliyojengwa eneo la Nangombo imeendelea kuwa tegemeo kubwa kwa wakazi wa wilaya na nchi jirani ya Msumbiji .
Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dr.Hussein Ngaillah anasema Hospitali hii, iliyoanza kutoa huduma rasmi mnamo Juni 2021, imeleta mapinduzi makubwa katika sekta ya afya, ikihudumia kata 20 zenye jumla ya wakazi 191,193, wakiwemo wanawake 93,494 na wanaume 97,699, pamoja na vijiji vya jirani kutoka Halmashauri ya mji wa Mbinga na nchi jirani ya Msumbiji.
HUDUMA ZINAZOPATIKANA
Kwa kipindi cha takriban miaka mitatu tangu kuanzishwa kwake, Hospitali ya Nyasa imefanikiwa kutoa huduma mbalimbali muhimu kwa jamii.
Huduma hizi ni pamoja na wagonjwa wa nje (OPD), wagonjwa wa ndani (IPD), huduma za maabara, afya ya uzazi na mtoto (RCH), dawa na vifaa tiba, huduma za mionzi kama X-ray na Ultrasound, afya ya kinywa na meno, fiziotherapia, na matibabu ya dharura (EMD).
Zaidi ya hayo, hospitali inatoa huduma za afya msonge, ikiwemo matibabu ya kifua kikuu na ukoma, tohara kwa wanaume, uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi, pamoja na chanjo mbalimbali kama ile ya homa ya ini na chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi.
ONGEZEKO LA WAGONJWA NA MAENDELEO YA HUDUMA
Tangu kuanzishwa kwake, hospitali hii imekuwa ikishuhudia ongezeko kubwa la wagonjwa wanaohudumiwa. Katika mwaka wa fedha 2020/2021, hospitali ilihudumia wagonjwa 195 pekee.
Hata hivyo, idadi hii iliongezeka maradufu mwaka wa fedha 2021/2022 kufikia wagonjwa 3,325. Mwaka uliofuata wa 2022/2023 idadi iliongezeka hadi wagonjwa 6,907, na mwaka wa fedha 2023/2024 hospitali ilihudumia wagonjwa 10,374. Ongezeko hili linaonesha jinsi hospitali hii inavyoendelea kuwa tegemeo kubwa kwa jamii.
UJENZI NA MAENDELEO YA MIUNDOMBINU
Hospitali ya Wilaya ya Nyasa imekuwa ikipanuka kwa awamu tatu chini ya mfumo wa Force Account, kwa kutumia jumla ya shilingi 3,391,376,520.00 kutoka Serikali Kuu.
Awamu ya Kwanza (2018/2019): Ujenzi wa majengo saba ukiwemo jengo la utawala, jengo la wazazi, jengo la wagonjwa wa nje, huduma za mionzi, ufuaji, stoo ya dawa na maabara kwa gharama ya shilingi 1,800,000,000.00.
Awamu ya Pili (2020/2021): Ujenzi wa wodi tatu (watoto, wanawake, na wanaume) pamoja na kichomea taka kwa gharama ya shilingi 491,376,520.00.
Awamu ya Tatu (2021/2022): Ujenzi wa jengo la upasuaji, wodi za upasuaji kwa wanaume na wanawake, jengo la kuhifadhi maiti, na jengo la huduma za dharura (EMD), kwa jumla ya shilingi 1,100,000,000.00 kutoka Mfuko wa Maendeleo wa Taifa wa UVIKO-19 (IMF).
UJENZI WA KITUO CHA KUFUA HEWA TIBA (OXYGEN PLANT)
Katika mwaka wa fedha 2023/2024, hospitali hii ilipokea mradi mkubwa wa uzalishaji wa hewa tiba (Oxygen Plant), uliotekelezwa na Serikali Kuu kupitia Wizara ya Afya na OR-TAMISEMI kwa gharama ya shilingi 409,000,000.00. Ufungaji wa mfumo huu ulifanywa na kampuni ya Tanzania Oxygen Gases Ltd, ukihusisha majengo ya huduma za dharura, wodi za upasuaji, na jengo la wazazi.
UWEKEZAJI KATIKA VIFAA TIBA
Katika kuhakikisha huduma bora zinaendelea kutolewa, Serikali imewekeza shilingi 1,208,105,000.00 katika ununuzi wa vifaa tiba kupitia Bohari Kuu ya Dawa (MSD).
Mwaka wa fedha 2021/2022: Vifaa vyenye thamani ya shilingi 490,000,000.00 vilinunuliwa
Mwaka wa fedha 2023/2024: Vifaa vya shilingi 418,105,300.00 kwa ajili ya jengo la EMD na Mwaka wa fedha 2024/2025: Vifaa vya shilingi 300,000,000.00 vinatarajiwa kusambazwa.
Hospitali ya Wilaya ya Nyasa imepiga hatua kubwa katika kutoa huduma bora kwa wananchi, huku Serikali ikiendelea kuwekeza katika miundombinu na vifaa tiba.
Kwa maendeleo haya yanayoendelea, ni dhahiri kuwa Hospitali ya Wilaya ya Nyasa inaelekea kuwa moja ya hospitali za kisasa zinazotoa huduma bora kwa wananchi, ikiwa ni matokeo ya jitihada kubwa za uwekezaji uliofanywa na Serikali .
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.