SERIKALI imekamilisha ujenzi wa majengo nane ya hospitali ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma ambapo kazi iliyokuwa imebaki ya kuunganisha mfumo wa umeme na maji safi imekamilika.
Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo Dr.Godwin Luta anasema Halmashauri hiyo,imekamilisha ujenzi wa hospitali ya wilaya ambao umetokana na jitihada za serikali ya awamu ya Tano za kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma ya matibabu jirani na maeneo wanayoishi.
Serikali inayoongozwa na Rais Dkt.John Magufuli imedhamiria kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi na kuwekwa msisitizo kwenye ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015 ambapo hadi sasa vimejengwa vituo vya afya na hospitali katika maeneo mbalimbali nchini.
“Ujenzi huu umefanyika kwa awamu tano ambapo kwa mwaka 2010/2011,Halmashauri yetu ilipokea fedha kutoka serikali kuu kiasi cha shilingi milioni 450 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala na wagonjwa wa nje’’,anasema Dr. Luta.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo Venance Nachimbinya anabainisha zaidi kuwa kati ya fedha zilizotolewa,katika jengo la wodi ya wazazi zimetumika zaidi ya shilingi milioni 176 na jengo la wodi ya wanaume zimetumika zaidi ya shilingi milioni 259.
Anabainisha zaidi kuwa jengo la upasuaji limegharimu zaidi ya shilingi milioni 213,jengo la stoo ya dawa zaidi ya shilingi milioni 203,jengo la maabara milioni 164,jengo la kufulia zaidi ya milioni 113,jengo la mionzi zaidi ya milioni 136,jengo la wodi ya wanawake zaidi ya milioni 166 na jengo la watoto zaidi ya milioni10.
Christina Mndeme ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma anawaagiza watendaji wa Halmashauri ya Namtumbo kuhakikisha majengo yaliyokamilika yanaanza kutumika kutoa huduma kwa wananchi wa Namtumbo ili kutimiza azma ya serikali ya kusogeza huduma ya afya karibu na wananchi.
“Wananchi hawataki kuona majengo. Badala yake wanataka kupata huduma za afya katika hospitali ,serikali imetekeleza wajibu wake wa kutoa fedha za kukamilkisha ujenzi ’’,anasisitiza Mkuu wa Mkoa.
John Milazi Mkazi wa Namabengo anasema kutekelezwa kwa mradi huo kunamfanya ajisikie amani kwa sababu akinamama na watoto kwa miaka mingi walikuwa wanapata shida ambapo hivi sasa serikali imewakumbuka kwa kuwajengea hospitali yenye huduma zote muhimu.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Septemba Mosi,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.